Marekani yaitaarifu UN juu ya uamuzi wake wa kujitoa mkataba wa Paris

4 Novemba 2019

Umoja wa Mataifa umesema umepokea barua kutoka Marekani ikielezea uamuzi wake wa kujitoa rasmi kwenye mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2015.

Taarifa kwa waandishi wa habari iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani imesema kuwa mchakato wa kujitoa unaanza leo tarehe 4 Novemba mwaka 2019 na utakamilika rasmi tarehe 04 Novemba mwaka 2020, ikiwa ni kwa mujibu wa kanuni za mkataba huo.

Marekani ilitia saini mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi tarehe 22 mwezi Aprili mwaka 2016 na tarehe 3 Septemba mwaka 2016 ikaelezea kuwa itazingatia yaliyomo kwenye mkataba huo katika kudhibiti mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa vipengele vya ibara ya 28 ya mkataba huo, aya ya 1, Marekani inaweza kujitoa kuanzia leo ali mradi iwasilishe notisi kwa Katibu Mkuu ambaye ni mhifadhi mkuu wa mikataba ya kimataifa.

Katika barua  yake kwa Katibu Mkuu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amesema kuwa,“barua hii ni notisi ya Marekani ya kujitoa kwenye mkataba wa Paris. Kwa mujibu wa Ibara ya 28, aya ya 2 ya mkataba wa Paris, kujitoa kwa Marekani kutaanza mwa mmoja kuanzia tarehe ambayo umepokea barua hii ya notisi ya kujitoa.”

Kwa mantiki hiyo, ifikapo tarehe 4 Novemba mwaka 2020 Marekani itakuwa si tena mwanachama wa mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter