Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mvutano wa China na Marekani kibiashara waumiza wananchi wao- UNCTAD

Vita vya kibiashara kati ya Marekani na China vimesababisha baadhi ya bidhaa za China kutoingia Marekani na mataifa mengine kunufaika na tafrani hiyo.
© MSC shipping
Vita vya kibiashara kati ya Marekani na China vimesababisha baadhi ya bidhaa za China kutoingia Marekani na mataifa mengine kunufaika na tafrani hiyo.

Mvutano wa China na Marekani kibiashara waumiza wananchi wao- UNCTAD

Ukuaji wa Kiuchumi

Msemo wa wahenga ya kwamba wapiganapo mafahali wawili ziumiazo ni nyasi, sasa imebainika vinginevyo katika vuta nikuvute ya ushuru kati ya Marekani na China ambapo Umoja wa Mataifa umesema mafahali  hao wawili ndio wanaoumia zaidi na wananchi wao.

Ripoti mpya ya Kamati ya Biashara na Maaendeleo ya Umoja wa Mataifa,  UNCTAD iliiyotolewa hii leo imesema kuwa vita vya kibiashara kati ya China na Marekani imesababisha kuporomoka kwa kiasi kikubwa kwa kiwango cha biashara kati yao huku wateja wakilipa bei za juu za bidhaa na ongezeko la ununuzi wa bidhaa kutoka mataifa yasiyohusika na vita hivyo.

Taarifa ya UNCTAD iliyotolewa leo Geneva, Uswisi imesema utafiti wa hivi karibuni umebaini kuwa wanunuzi nchini Marekani wanabeba mzigo ongezeko la  ushuru wa bidhaa uliowekwa na Marekani kwa bidhaa zitokazo China kwa kuwa hivi sasa ongezeko la bei linahamishiwa kwa kampuni zinazoagiza bidhaa.

Hata hivyo utafiti huo umebaini pia kwamba kampuni za China zimeanza kubeba gharama za ongezeko la  ushuru kwa kupunguza bei za bidhaa zao wanazouza nje ya nchi.

 “Matokeo ya utafiti huu ni onyo kwa dunia. Kuingia hasara kwa pande zote mbili zilizopo kwenye mvutano wa kibiashara, si tatizo tu kwa pande mbili hizo bali pia kunaleta madhara kwenye utulivu wa uchumi duniani na kwa siku zijazo,” amesema Pamela Coke Hamilton, Mkurugenzi wa biashara ya kimataifa na bidhaa, UNCTAD.

Bi. Hamilton amesema ni matumaini  yao kuwa mkataba wa biashara kati ya China na Marekani unaweza kupunguza mvutano unaoendelea hivi sasa.

Uchambuzi wa takwimu unaonesha kuwa ushuru wa Marekani umesababisha kuporomoka kwa asilimia 25 ya mauzo ya bidhaa za nje na kuathiri thamani ya bidhaa kutoka China zenye thamani ya dola bilioni 35 katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2019 pekee.

Wakati Taiwan na Mexico zinanufaika na vita vya kibiashara kati ya China na Marekani, nchi za Afrika zimeambulia patupu- Ripoti UNCTAD

Hata hivyo takwimu zinadhihirisha kiwango cha  juu cha ushindani cha kampuni za China ambazo licha ya kuwepo kwa ushuru zimeendelea kuuza asilimia 75 za bidhaa zao nchini Marekani.

Sekta zilizoathirika vibaya zaidi ni zile za vifaa vya mitambo na mawasiliano ambapo uagizaji wake kutoka China kuingia Marekani umepungua kwa dola bilioni 15.

Bidhaa nyingine zilizopungua kuagizwa na Marekani kutoka China kutokana na ongezeko la ushuru ni kemikali, samani na mitambo ya umeme.

Ingawa utafiti huo  haukuchunguza athari za awamu ya hivi karibuni zaidi ya mvutano wa kibiashara kati ya pande mbili hizo, UNCTAD inaonya kuwa mwendelezo wa mvutano wakati wa msimu wa majira ya joto mwaka huu unaweza kuwa umesababisha hasara ambazo kampuni za China imepata.

Wakati China inapata hasara, mataifa mengine yamenufaika

Ushuru wa bidhaa za China chini Marekani umekuwa na faida kwa wengineo kwa kuwa kati ya dola bilioni 35 za bidhaa za China ambazo hazikungia Marekani, asilimia 63 ya kiwango hicho ilielekezwa mataifa mengine.

Mathalani Taiwan iliuza zaidi bidhaa za Marekani zenye thaman iya dola bilioni 4.2 ikiwa ni katika bidhaa za mitambo na mawasiliano.

Mexico nayo iliongeze mauzo yake ya bidhaa Marekani kwa dola bilioni 3.5, ikiwa ni mazao ya chakula kutokana na kilimo, vifaa vya usafirishaji na mitambo ya umeme.

Hata hivyo nchi za kiafrika  hazikunufaika na mvutano huo.