Tuwekeze kwenye miradi inayohimili Tsunami- Guterres

Katika maeneo ya ukanda wa chini wa pwani huko Vanuatu, wanafunzi wakifanya zoezi la kujiandaa dhidi ya mawimbi ya Tsunami
UNDP
Katika maeneo ya ukanda wa chini wa pwani huko Vanuatu, wanafunzi wakifanya zoezi la kujiandaa dhidi ya mawimbi ya Tsunami

Tuwekeze kwenye miradi inayohimili Tsunami- Guterres

Tabianchi na mazingira

Harakati za kupunguza madhara yatokanayo na mawimbi ya Tsunami ni muhimu ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres  katika maadhimisho ya siku ya kuhamasisha uelewa wa Tsunami duniani hii leo.

Maadhimisho haya yanafanyika ikiwa ni miaka 15 tangu tetemeko la ardhi chini ya bahari liliposababisha mawimbi ya Tsunami katika bahari ya Hindi na kutikisa  mataifa 14 huku watu 230,000 wakifariki dunia.

Katika ujumbe wake huo , Bwana Guterres amesema tangu wakati huo, “tumeshuhudia kuimarika kwa mifumo ya kutoa onyo sit u katika bahari ya Pasifiki, bali pia katika bahari ya Hindi, Karibea, maeneo ya kaskazini-mashariki mwa Atlantiki, Mediteranea na kwingineko.”

Hata hivyo amesema ni dhahiri kwa kuzingatia hasara za kiuchumi zilizopatikana katika miaka 20 iliyopita, “bado hatujajifunza vyema juu ya umuhimu wa kuwa na miundombinu yenye mnepo dhidi ya tsunami. Hii ni muhimu sana ili kuepusha kuharibiwa kwa mifumo ya huduma kwa umma, uharibifu ambao unaweza kutokea wakat iwa Tsunami, tetemeko la ardhi na matukio ya kupindukia ya hali ya hewa.”

Kituo cha kitamaduni huko Chamanga nchini Ecuador, ambacho ubunifu wake ukiwa ni baada ya tetemeko la ardhi la mwaka 2016
Center for Public Interest Design
Kituo cha kitamaduni huko Chamanga nchini Ecuador, ambacho ubunifu wake ukiwa ni baada ya tetemeko la ardhi la mwaka 2016

Bwana Guterres anaonya kuwa harati bado ni kubwa akisema kwamba tarkibani watu milioni 680 wanaishi kwenye ukanda wa pwani ulio chini na kwamba ifikapo mwaka 2050, idadi ya watu hao itavuta bilioni 1.

“Wakati huo huo, kiwango cha maji ya bahari kinaongezeka kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaweza kuchochea zaidi uthabiti wa Tsunami,” amesema Katibu Mkuu.

NI kwa mantiki hiyo amesema kuwa harakati zozote za kupunguza madhara zitakuwa muhimu ili kufanikisha SDGs na hivyo basi, “katika siku hii ya kujenga uelewa kuhusu Tsunami, nasihi serikali, mamlaka za mitaa na sekta ya ujenzi zisake maendeleo yanayotambua madhara na kuwekeza katika mnepo.”

Baraza Kuu nalo laadhimisha siku ya uhamasishaji kuhusu Tsunami

Katika makao makuu ya  Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Muhammad Tijan-Bande ameongoza kikao maalum kilichokutana kuadhimisha siku ya kuelimisha jamii kuhusu tsunami.

Tukio hilo liliandaliwa na Uwakilishi wa Kudumu wa Japan kwenye Umoja wa Mataifa, kundi la marafiki la kupunguza madhara ya majanga, shirika la mpango wa  maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza madhara ya majanga, UNDRR.

Uharibifu baada ya tsunami kupiga Japan
Ewerthon Tobace
Uharibifu baada ya tsunami kupiga Japan

Akizungumza kwenye tukio hilo, Profesa Bande amesema, “katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili iliyopita, zaidi ya watu 250,000 wamepoteza maisha kutokana na mawimbi ya tsunami. Leo tunapoadhimisha siku hii tunawakumbuka na kuhakikisha kuwa kupotea kwa maisha yao hakutaishia tu hivi hivi, bali tutachukua hatua.”

Rais huyo wa Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa amesihi nchi wanachama zitekeleze mikakati ya kupunguza madhara ya majanga ili kulinda vizazi vijavyo.

Pamoja na watu kupoteza maisha, Profesa Bande amesema katika miongo hiyo miwili, tsunami imesababisha asilimia 10 ya hasara za kiuchumi na kwamba, “hasara hizi zimerudisha nyuma maendeleo yaliyopatikana na kuongeza mzigo wa madeni kwa nchi hususan zile zilizoko bahari ya Hindi.”

Amesema akiangazia jinsi ya kupunguza madhara yatokanayo na majanga, anaona kupitia lensi  ya vipaumbele vya mkutano wa 74 wa Baraza Kuu anaoongoza, vipaumbele ambavyo ni lazima vilindwe kwa kupunguza madhara  ya majanga.

Vipaumbele hivyo ni amani na usalama, kupitia uzuiaji wa mizozo, kutokomeza umaskini, kutokomeza njaa, hatua kwa tabianchi, kupata elimu bora na  ujumuishi na kwamba mafanikio yoyote katika vipaumbele hivyo yanaweza kufutwa na tukio moja tu la janga kubwa.

Amekumbusha washiriki kuwa tayari mataifa ya mbinu muhimu ya kupunguza madhara ya majanga ambayo ni mkataba wa Paris wa mwaka 2015 wa  kudhibiti majanga, malengo ya maendeleo endelevu, SDG na mfumo wa Sendai wa kupunguza madhara ya majanga.