Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN na wadau walaani shambulio Ituri lililosababisha kifo cha mhudumu wa kijamii

Mhudumu wa afya anayehusika na kuhudumia wagonjwa wa Ebola akiwa amevalia mavazi sahihi ya kujikinga huku akimlisha mtoto kwenye kituo cha tiba dhidi ya Ebola huko Kivu Kaskazini nchini DRC. ( 30 januari 2019)
WFP/Jacques David
Mhudumu wa afya anayehusika na kuhudumia wagonjwa wa Ebola akiwa amevalia mavazi sahihi ya kujikinga huku akimlisha mtoto kwenye kituo cha tiba dhidi ya Ebola huko Kivu Kaskazini nchini DRC. ( 30 januari 2019)

UN na wadau walaani shambulio Ituri lililosababisha kifo cha mhudumu wa kijamii

Afya

Kamati ya kiufundi ya kukabili Ebola nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC sambamba na Wizara ya Afya na mashirika ya Umoja wa Mataifa wamelaani vikali ghasia za jana huko jimboni Ituri ambazo zimesababisha kifo na majeruhi. 

Ghasia hizo katika eneo la Lwemba jimboni Ituri, kaskazini-mashariki mwa DRC zimesababisha kifo cha mfanyakazi wa kijamii ambaye alikuwa mstari wa mbele kukabili mlipuko wa Ebola huku mkewe akipata majeruhiwa makubwa.

Taarifa iliyotolewa Goma, Kivu Kaskazini na shirika la afya  ulimwenguni, WHO kanda ya Afrika imesema mfanyakazi huyo alikuwa pia mwanahabari wa kituo cha radio ya jamii huko Lwemba na alihusika sana kuhamasisha jamii kuhusu mlipuko huo wa 10 wa Ebola nchini humo ambao ulianza mwaka mmoja uliopita kwenye majimbo ya Ituri, Kivu Kusini na Kivu Kaskazini.

Ingawa washukiwa wawili wamekamatwa, dadi sasa sababu ya shambulio hilo haijafahamika huku mamlaka zikiwa tayari zimeanza uchunguzi kuona iwapo shambulio hilo lina uhusiano na harakati dhidi ya Ebola.

WHO imesema kuwa tukio lolote la ghasia dhidi ya watu wanaokabiliana na Ebola halikubaliki na linakwamisha uwezo wa wafanyakazi hao kuhudumia jamii zilizoathirika kwa Ebola.

Halikadhalika imesema mamlaka zote za usalama ikiwemo polisi, usalama wataifa na jeshi wanashirikiana kuhakikisha watekelezaji wanafikishwa mbele ya sheria haraka iwezekanavyo.

Sekretarieti ya kamati ya kiufundi dhidi ya Ebola, sambamba na Wizara ya Afya na wadau kutoka Umoaj wa Mataifa ambao ni WHO, UNICEF na kikosi kazi cha operesheni dhidi ya Ebola, UNEERO wametuma salamu za rambirambi kwa wafiwa na jamii zilizoathirika.

Tangu tarehe Mosi mwezi Januari mwaka huu, WHO imerekodi zaidi ya mashambulizi 300 kwenye vituo vya afya nchini DRC ambayo yamesababisha vifo vya watu 6 na majeruhi 70, ikiwa ni wahudumu wa afya na wagonjwa.

Kwa mujibu wa WHO, kila shambulio ni kikwazo kwa hatua dhidi ya Ebola kwa kuzingatia kuwa bila usalama, timu za tiba na usaidizi haziwezi kufikia wanajamii.