Guterres bado ana hofu kuhusu Myanmar, ataka hatua zaidi ASEAN

3 Novemba 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema bado anaendelea kuwa na wasiwasi mkubwa juu ya hali ya Myanmar, ikiwemo jimboni Rakhine sambamba na idadi kubwa ya wakimbizi wa taifa hilo wanaoishi katika mazingira magumu.

Guterres amesema hayo huko Bangkok, Thailand wakati akihutubia mkutano wa 10 wa ngazi ya juu kati ya Umoja wa Mataifa na jumuiya ya nchi za kusini-mashariki mwa Asia, ASEAN.

“Inasalia bila shaka kuwa ni wajibu wa Mynmar kushughulikia visababishi vya raia kukimbia jimboni Rakhine na kuhakikisha kuwa kuna mazingira salama kwa wakimbizi kurejea nyumbani kwa hiari, kwa utu na kwa uendelevu huko jimboni Rakhine, na hivyo vifanyike kwa mujibu wa sheria za kimataifa,” amesema Katibu Mkuu.
 
Ametaja mambo ya kuzingatia kuwa ni pamoja na taifa hilo kuwezesha kufanyika kwa mazungumzo na wakimbizi na kuweka mazingira ya kurejea kwa imani.

Halikadhalika kuridhia bila kuchelewa miradi ya matokeo ya haraka ya kuwezesha wakimbizi wanaorejea kuwa na njia za kujipatia kipato sambamba na miundombinu, huduma za msingi na za ulinzi na usalama, “na kuharakisha suluhu kwa wale ambao bado wamesalia kuwa wakimbizi wa ndani nchini humo.”

Warohingya ambao ni kabila kutoka jimbo la Rakhine nchini Myanmar, hawana uraia na hawana utambulisho wowote. Hapa ni Cox's Bazar nchini Bangladesh wakiwa hawajui hatma ya kurejea nchini mwao.
K M Asad/UN
Warohingya ambao ni kabila kutoka jimbo la Rakhine nchini Myanmar, hawana uraia na hawana utambulisho wowote. Hapa ni Cox's Bazar nchini Bangladesh wakiwa hawajui hatma ya kurejea nchini mwao.

Katibu Mkuu amesema hatua zote hizo ni lazima zizingatie mapendekezo ya Kamisheni ya Ushauri kwa jimbo la Rakhine ambayo itahitaji kufuatilia kwa umakini.

Hata hivyo ametumia hotuba yake kukaribisha hatua za hivi karibuni za ASEAN kushauriana na Myanmar na amesihi juhudi hizo ziendelee.

Baada ya kuhutubia mkutano huo, Katibu Mkuu alikuwa na mkutano na waandishi wa habari ambapo aliulizwa swali kuhusu mustakabali wa wakimbizi wa Rohingya na juhudi za ASEAN katika kushughulikia suala hilo ambapo amesema kuwa, “alijulishwa kuwa ASEAN inashauriana kwa karibu zaidi na serikali ya Myanmar na kwamba kuna kikosi kazi maalum kimeundwa kufuatilia juhudi hizo.”

Hata hivyo amesema jambo muhimu zaidi ni kuweka mazingira ya kuwepo kwa maridhiaono ya dhati baina ya jamii.

“Katika jimbo la Rakhine kuna jamii ya warohingya. Ni muhimu kuweka mazingira ya maridhiano ya kuwezesha kutokomezwa kwa kauli za chuki, kuwezesha kutoweka kwa kauli za chuki na wengine kukataliwa, na vikosi vya jeshi na polisi viwe chachu ya maridhiano na si visababishi vya mateso, ili hatimaye watu wajihisi wako salama kurejeah nyumbani na wanaerejea kwa utu na kwa hiari,” amesema Katibu Mkuu.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter