UN na Uturuki zapigia chepuo Kamati ya Kikatiba ya Syria

1 Novemba 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyeko ziarani nchini Uturuki, hii leo amekuwa na mazungumzo na Rais wa nchi hiyo Recep Tayyip Erdoğan ambapo amemshukuru kwa dhati jinsi taifa hilo linavyoshirikiana na Umoja wa Mataifa.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa hii leo huko Instanbul Uturuki, imesema kuwa, “viongozi hao wawili wameelezea kwa pamoja kuunga mkono vikao vinavyoendelea vya kamati ya kikatiba ya Syria na umuhimu wa kusaka suluhu ya kisiasa ya mzozo wa Syria sambamba na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 2254.”

Wakati wa mazungumzo hayo, Rais Erdoğan amemkabidhi Katibu Mkuu mpango wa Uturuki wa makazi mapya kwa ajili ya wakimbizi wa Syria wanaorejea nyumbani.

Katibu Mkuu Guterres amesisitiza kanuni ya msingi ya kuhakikisha kuwa kurejea huok kunakuwa ni kwa hiari, salama na kufanyike kwa utu.

Aidha amemweleza Rais Erdoğan kuwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, litaanda mara moja timu ya kutathmini mpango huo na kufanya mashauriano na mamlaka ya Uturuki kwa mujibu wa majukumu ya shirika hilo.

Viongozi hao wawili walibadilishana mawazo kuhusu hali ya mchakato wa amani Mashariki ya Kati pamoja na Yemen na Libya sambamba na masuala mengine ya kimataifa yanayohusu Umoja wa Mataifa na Uturuki.

Bwana Guterres amesisitiza kuunga mkono pia nyaraka ya maelewano kati ya Uturuki na kundi la wadau wa maendeleo kuhusiana na usaidizi wa Uturuki katika hatua zake dhiti ya mabadiliko ya tabianchi.

Halikadhalika Katibu Mkuu amempatia muhtasari rais huyo wa Uturuki juu ya ziara  yake kwenye benki ya teknolojia ya Umoja wa Mataifa na kushukuru Uturuki kwa kuwa mwenyeji wa benki hiyo na ufadhili wa chombo hicho.

Hata hivyo Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa kuongeza usaidizi wa kimataifa kwenye benki hiyo inayosaidia nchi zinazoendelea kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu.

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter