Winnie Byanyima aanza kazi rasmi kama mkuu wa UNAIDS

Winnie Byanyima ambaye ni mkurugenzi mtendaji mpya wa UNAIDS
UN Photo/Amanda Voisard
Winnie Byanyima ambaye ni mkurugenzi mtendaji mpya wa UNAIDS

Winnie Byanyima aanza kazi rasmi kama mkuu wa UNAIDS

Afya

Winnie Byanyima kutoka nchini Uganda leo ameanza kazi rasmi ya Mkurugenzi Mtendaji mpya wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya ukimwi UNAIDS. Brenda Mbaitsa na taarifa kamili.

Bi. Byanyima anaingia katika shirika la UNAIDS akiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 30 katika uongozi wa kisiasa, kidiplomasia na kujihusisha na masuala ya kibinadamu. Akizungumzia jukumu hilo jipya baada ya kuwasili ofisini kwake Bi. Byanyima amesema “Nimefurahi sana kujiungana UNAIDS na ninatarajia kufanya kazi na wengine ulimwenguni kote katika kusongesha juhudi za kukabiliana na VVU na Ukimwi, na kujenga jamii zenye afya na furaha, haswa kwa wanawake na wasichana na kwa vikundi vyote vya watu walioachwa nyuma au kusahaulika. "

Byanyima amekuja na uzoefu mkubwa na wa miaka mingi na dhamira ya kutumia uwezo wa serikali, mashirika, sekta binabfi na asasi za kiraia ili kusukuma mbele ajenda ya maendeleo inayojikita katika matakwa ya watu.

Kabla ya kujiunga na shirika la UNAIDS Byanima alikuwa mkurugenzi mtendaji wa shirika la kimataigfa la Oxfam na pia alihudumua kwa miaka saba kama mkurugenzi wa masuala ya jinsia na maendeleo katika shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP.

Bi. Byanyima ana shahada ya juu katika uhandisi wa mitambo kutoka Taasisi ya Teknolojia ya Cranfield na ana shahada ya uzamili katika uhandisi wa masuala ya  ndege na anga kutoka Chuo Kikuu cha Manchester.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antoniuo Guterres alimteua Bi. Byanyima kuwa msaidizi wa Katibu Mkuu na mkurugenzi mtendaji wa UNAIDS mwezi Agosti mwaka huu 2019, kufuatia mchakato wa kina wa uteuzi uliohusisha wajumbe wa kamati ya bodi ya UNAIDS . Na kamati ya ufadhili mwenza wa UNAIDS ndiyo iliyofanya  na kutoa mapendekezo ya mwisho ya uteuzi wake kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.