Somalia yachukua hatua kulinda haki za mtoto

31 Oktoba 2019

Serikali ya Somalia  imerejelea ahadi yake ya kutokomeza kitendo cha kuandikisha watoto kwenye jeshi ambapo imetia saini nyaraka inayoeleza kinagaubaga hatua za kuzuia kitendo hicho.

Kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto na mizozo ya kivita, Virginia Gamba akiwa ziarani kwenye pembe hiyo ya Afrika amekutana na maafisa waandamizi wa serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Ulinzi Hassan Ali Mohamed,

Ni katika mkutano huo ambapo Waziri huyo kwa niaba ya serikali walitia saini nyaraka hiyo ikionesha hatua za kuzuia ukiukaji wa haki za mtoto, kuachilia huru watoto wanaotumikishwa jeshini na kuwajumuisha kwenye jamii.

Nyaraka iliyotiwa saini ni sambamba na mpango wa utekelezaji uliotiwa saini kati ya Somalia na Umoja wa Mataifa mwaka 2012 kwa lengo la kulinda watoto wasitumikishwe jeshini.

Bi. Gamba akiwa ni shuhuda amesema,"Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia yenye nia njema yataunga mkono mpango huu ili kote Somalia, maafisa wote wa kusimamia sheria na wanajeshi wote wawe watu wa kwanza kulinda watoto. Na katika hili tutaunga mkono suala la kuchunguza na kujengea uwezo na kuhakikisha kuwa watoto ambao wanakamatwa, au wanatoroka au watoto ambao wanaachiliwa huru nao pia wanapata msaada ya kuwaraghibisha, kuwajumuisha na kuwapatia mahitaji yao.

Kwa upande wake, Waziri Mohamed amesisitiza azma ya serikali ya Somalia ya kutokomeza ukiukwaji haki za watoto ikiwemo utumikishwaji jeshini.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwezi Juni mwaka huu ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto kwenye mizozo ya vita, vikundi vilivyojihami Somalia vilitumikisha vitani wavulana 2,228 na wasichana 72.

Al-Shabaab pekee ilitumikisha watoto 1,865 , ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya watoto askari.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter