Magaidi 7 wa ISIS walinibaka kwa zamu nikiwa na umri wa miaka 14, nataka haki itendeke- Manusura

(Kushoto- Kulia) Naledi Pandor, Waziri wa Mambo ya Nje Afrika Kusini, Nadia Murad, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Pramila Patten, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN kuhusu ukatili wa kingono na Dkt. Denis Mukwege mshindi wa tuzo ya Nobel
UN Photo/Mark Garten)
(Kushoto- Kulia) Naledi Pandor, Waziri wa Mambo ya Nje Afrika Kusini, Nadia Murad, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Pramila Patten, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN kuhusu ukatili wa kingono na Dkt. Denis Mukwege mshindi wa tuzo ya Nobel

Magaidi 7 wa ISIS walinibaka kwa zamu nikiwa na umri wa miaka 14, nataka haki itendeke- Manusura

Amani na Usalama

Hii leo katika kuadhimisha miaka 19 tangu kupitishwa kwa azimio namba 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia ukatili wa kingono kwenye mizozo, manusura wa ukatili huo wametoa shuhuda dhahiri za yale waliyopitia huku wakitaka hatua thabiti za usaidizi na uwajibishwaji wa waliowatendea makosa.

Tukio hilo limefanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, ambapo miongoni mwa waliozungumza ni Badrya Fayez Omar kutoka Iraq ambaye amesema, “nilikuwa na umri wa miaka 14 wakati nilipotekwa na magaidi wa kikundi cha ISIS ambao magaidi 7 walinibaka kwa zamu.”

Akizungumza huku akionekana kujizuia kutokwa na machozi, Badrya amesema, “nashangaa sana kwa kuwa nilitoa ushahidi mbele ya kamati ya uchunguzi wa maovu  yaliyofanywa na ISIS na hata kuelezea muonekano wa watu hao walionibaka lakini hadi leo hakuna chochote kilichofanyika.”

Badrya amesema kuwa hata sasa nduguze wawili bado wanashikiliwa na ISIS na kila mara anapoenda mjini Mosul, bado anahisi jinamizi kuwa huenda atakutana na watu hao waliomtendea maovu.

Kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Tatiana Mukanire, manusura ambaye amesema anazungumza kuwakilisha maelfu ya wanawake waliobakwa kwenye taifa hilo lililogubikwa na mzozo, amesema kuwa msaada wa kiuchumi uende sambamba na fidia na kuwachukulia hatua wale waliowabaka.

Bi. Mukanire ambaye anaongoza kikundi cha vuguvugu la kitaifa la manusura wa ukatili wa kingono nchini DRC katika hotuba yake hiyo ametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa akisema, "mataifa ambayo yameahidi kusaidia manusura basi tekelezeni ahadi zenu ili angalau sisi tuweze kujenga maisha yetu."

 

Tatiana Mukanire, ni mratibu wa vuguvugu la kitaifa la manusura wa ukatili wa kingono, DRC.
UN News/ Cristina Silveiro
Tatiana Mukanire, ni mratibu wa vuguvugu la kitaifa la manusura wa ukatili wa kingono, DRC.

Manusura kutoka Sudan Kusini

Kutoka Sudan Kusini, manusura mbaye alitoa ushuhuda kwa njia ya video na jina lake kuhifadhiwa amesema, “mwezi Julai mwaka 2016 tukiwa tunakwenda kuchanja kuni na wanawake wenzangu 7 tulibakwa  mara kwa mara na watu waliokuwa wamevalia sare za kikundi cha Sudan Peoples Liberation Army, SPLA na sare za shirika la wanyamapori la Sudan Kusini.”

Manusura  huyo mwenye  umri wa miaka 36 na mama watoto 6, amesema walikuwa wamesaka hifadhi kwenye kituo cha uhifadhi wa raia cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS mjini Juba, lakini walipoenda kusaka kuni ndipo walipobakwa na askari hao 7  mara kwa mara na yeye mwenyewe kujikuta amepata ujauzito.

“Hivi sasa sisi watatu ambao tulipata ujauzito na kuzaa watoto tunapata ugumu kuwalea bila baba zao. Hatuna cha kuwalisha na kuwakuza, hatuwezi hata kununua maziwa au mahitaji muhimu.  Ningalipenda kuungana na watoto wangu kwenye kambi  ya wakimbizi Ethiiopia. Hata hivyo baada ya mume wangu kusikia kuhusu kubakwa kwangu , amenikataa na amezuia mawasiliano yoyote na watoto.  Mimi ni mama wa watoto watatu wa kiume na wasichana wawili pamoja na huyu mmoja aliyezaliwa baada ya mimi kubakwa," amesema manusura huyo kupitia ujumbe wake huo uliokuwa umerekodiwa.

Manusura huyo amesema anataka waliombaka wachukuliwe hatua na kwamba, "niko tayari kutoa ushahidi popote pale mahakamani iwe Sudan Kusini au nje ili mradi wabaya wangu wafikishwe mbele ya sheria,”  amesema manusura huyo akikumbusha kuwa, "sisi manusura tunahitaji msaada. Sasa hivi sisi si chochote. Hatuna elimu, tumetelekezwa na jamii kwa kuwa wengi wetu hivi sasa hatukubaliwi tena na waume zetu."

Manusura huyo amesema hawana hata njia ya kujipatia kipato huku mume wake akimlaumu kwa kile kilichomfika akisema kuwa, "nitazeeka nikiwa tu na huyu mtoto ambaye amezaliwa baada ya mimi kubakwa. Ujumbe wangu kwa Baraza la Usalama ni kwamba jang a la Sudan Kusini sasa ni miaka 5, je hamjasikia kile kilichotufika hasa sisi wanawake wa Sudan Kusini? Niko  hapa kuwajulisha kuwa kuna wanawake wengi Sudan Kusini waliokumbwa na ukatili. Tunataka msaada kwa wahusika wafikishwe mbele ya sheria na pia mzozo wa Sudan Kusini umalizike. Watu wengine wanaugua ugonjwa wa akili, watu wanazungumzia amani kuja Sudan Kusini, iwapo mchakato hou unakufa, wanawake watabakwa. Kadi ya mgao ninayopata kwa ajili ya chakula hakitoshi. Nisingalikuwa nimebakwa ningalikuwa bado na utu wangu na ningaliendelea kujumuika na watoto wangu na kuendelea na maisha yangu."

Kufuatia shuhuda hizo, Dkt. Denis Mukwege, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel  mwaka 2018 na pia mwenyekiti wa taasisi ya Mukwege inayosaidia kutibu wanawake waliobakwa huko DRC aliwaambia washiriki kuwa, ni dhahiri baada ya kusikia kauli za manusura wa ukatili tumetambua kuwa sisi tuna wajibu mkubwa wa kibinadamu.”

Tusimulike tu raia, bali pia wanawake walinda amani nao wanakumbwa na ukatili

Kwa upande wake Dkt. Naledi Pandor ambaye ni Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini ametaka jumuiya ya kimataifa pamoja na kuangazia manusura wa ukatili wa kingono raia, wasisahau walinda amani wanawake ambao pia hukumbwa na ukatili wa kingono.

“Jana mlinda amani mmoja mwanamke alitoa ushuhuda jinsi ambavyo wakiwa kwenye operesheni za ulinzi wa amani yeye alinusurika kubakwa lakini kuna wengine walibakwa,”  hivyo amesema “tupatie wote kipaumbele.”

Dkt. Pandor ametaka pia mashirika ya kiraia kuwa makini kufuatilia ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambayo hutaja watuhumiwa au wahusika wa ukatili wa kingono ili kuhakikisha kuwa hawarejei tena kwenye majukumu yao na kutishia amani.

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed amekumbusha kuwa, “katu tusikubali ukatili wa kingono uwe ni jambo ambalo litaingia kwenye historia kama jambo ambalo halikuweza kuchukuliwa hatua.”

Amesema ni dhahiri kuwa vitendo vya jamii ya kimataifa haviendani na maneno na kwamba maazimio na sheria vitakuwa na maana kama ilivyo ahadi za kisiasa na kifedha katika kutekeleza hatua hizo.

Naye Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili wa kingono kwenye mizozo, Pramila Patten amesema kuna hatua zimechukuliwa ili kukabili vitendo hivyo, ikiwemo “walinzi wa amani kufundishwa vyema jinsi ya kushughulikia visa vya ukatili wa kingono.”

Wakati wa tukio hilo Dkt. Mukwege na mshindi mwenza wa tuzo ya amani ya Nobel, Nadia Murad, wametangaza uzinduzi wa mfuko wa kimataifa wa kusaidia manusura wa ukatili wa kingono.

Mfuko huo utasaidia manusura angalau kupata fidia ambapo Bi. Murad amesema, "fidia ni  haki na shinikizo ambavyo vinapaswa kuelekezwa kwa serikali ili ziweze kutekeleza wajibu wao. Fidia pia ni msaada kwa manusura ili waweze kuanza angalau kupona makovu. Fidia hufanya manusura waonekane, wasikike na watambuliwe. manusura hawawezi kuanza kujikusanya upya na kuanza maisha tena bila fidia."