Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua mliyochukua kamati ya katiba ya Syria ni matumaini kwa wasyria wote- UN

Syria, jimbo la Al-Hasakeh Oktoba 11, 2019, wanawake waliofurushwa wakisafiri kwa njia ya bara bara.
WFP/Alan Ali
Syria, jimbo la Al-Hasakeh Oktoba 11, 2019, wanawake waliofurushwa wakisafiri kwa njia ya bara bara.

Hatua mliyochukua kamati ya katiba ya Syria ni matumaini kwa wasyria wote- UN

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umesema hatua iliyochukuliwa na kamati ya katiba ya Syria kwa mara ya kwanza kuwakutanisha uso kwa uso serikali ya nchi hiyo na tume ya upinzani ya majadiliano  na pia asasi za kiraia ni hatua kubwa na muhimu kuelekea mustakabali wa taifa hilo.

Hatua hiyo ya leo ya kihistoria ya uzinduzi wa kamati ya katiba ya Syria  imekaribishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambaye  amesema makundi yote hayo kuketi pamoja ni muhimu katika kuchukua hatua ya kwanza katika mchakato wa kisiasa wa kuondokana na madhila ya mgogoro wa Syria.

Bwana Guterres amesema,  "nimeridhishwa pia kwamba uwakilishi wa wanawake katika kamti hiyo ni karibu asilimia 30. Ninatarajia kwamba pande zote zitashirikiana kwa roho safi kuelekea suluhu ya mgogoro wa Syria kwa kuzingatia azimio namba 2254 ambalo ni la kukidhi matakwa ya watu wote wa Syria kuhakikisha uhuru wao, umoja na mustakabali wao."

Naye Mwakilishi Maalum wa Umoja kwa suala la Syria, Geir O. Pedersen akizungumza kwenye mkutano huo wa kihistoria mjini Geneva Uswisi hii leo amesema anatambua kwamba si rahisi kwa pande zote hizo kukutana na kuketi kwa pamoja baada ya karibu miaka tisa ya vita, i ngawa bado kuna hisia za machungu, na tofauti anaheshimu sana uwepo wao.

Bwana Pedersen amesema, “lakini suala kwamba leo mpo pamoja mmeketi pamoja uso kwa uso tayari kuanza mazungumzo na mashauriano,  naamini ni ishara thabiti ya matumaini kwa wasyria kila mahali.”

Umoja wa Mataifa unasisitiza kwamba kuzinduliwa kwa kamati hityo leo na kazi zake ni lazima viende sambamba na hatua Madhubuti, kujenga uaminifu na kuweka mbele maslahi ya wasyria wote.