Jukumu la wanawake walinda amani kwenye mizozo ni zaidi ya kubeba mtutu- Tanzania

Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wanaofanya kazi na kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB cha Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, DRC, MONUSCO katika eneo la Beni, Mavivi jimbo la kivu Kaskazini.
©MONUSCO/FIB/Mohammed Mkumba
Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wanaofanya kazi na kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB cha Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, DRC, MONUSCO katika eneo la Beni, Mavivi jimbo la kivu Kaskazini.

Jukumu la wanawake walinda amani kwenye mizozo ni zaidi ya kubeba mtutu- Tanzania

Amani na Usalama

Mkutano kuhusu wanawake amani na usalama ukifanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani na kuleta shuhuda za wanawake walinzi wa amani na uzoefu wao kwenye uwanja wa mapambano hususan Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Tanzania imesema uzoefu huo ni ushahidi tosha kuwa jukumu la wanawake kwenye ulinzi wa amani ni zaidi ya kubeba mtutu wa bunduki.

Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Modest Mero, akizungumza na UN News Kiswahili baada ya kushiriki mkutano huo amesema, "hawa wanawake pamoja na kwamba wao ni askari, wanadhibiti mashambulizi hayo kijeshi, lakini pia  wanachukua hatua za ziada ya kujaribu kulinda watoto, wanakuta wengine hawajapata chakula, wanawapatia chakula, kwa sababu wanajisikia kuwa ni sawa na watoto wao. Lakini pia wanaona wanawake wanaoteseka katika vita ambavyo hawajavianzisha. Kwa hiyo na wao wanajaribu kuwasaidia kuanzisha miradi mbalimbali ili wajikimu katika suala  kubwa la umaskini.

Naye mwambata wa kijeshi kwenye uwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Kanali George Itang’are amesema Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kutoa mafunzo kwa maafisa na askari wa kike kutoka nchi za kigeni ambapo amesema kuwa, "Tanzania  ilichukua jukumu la kuendesha mafunzo , kwa mfano tuliendesha kozi ya maafisa wa Botswana na Swaziland. Hizi  ni nchi ambazo hazikuwahi kuwa na maafisa wa kike. Hata katika mfano uliotolewa, Malawi wamejaribu kuhesabau idadi ya maafisa wanne tu ambao wamewahi kushiriki kwenye operesheni za ulinzi wa amani. Kwa hivyo utaona kuwa hili agizo la kuongeza idadi ya wanawake katika ulinzi wa amani, sisi Tanzania vikosi vyetu vyote vina uwakilishi m zuri wa wanawake na inapokuja lile suala la kupeleka wanawake iwe ni waangalizi wa kijeshi, kwa kweli tunafikia ule uwiano uliowekwa na Umoja wa Mataifa."

Kanali Dokta Agatha-Mary Katua ni afisa kutoka jeshi la Tanzania na alikuwa mlinzi wa amani huko Sierra Leone kati ya mwaka 2003-2004 ambapo akisimulia uzoefu wake amesema kuwa, "wakati mwingine kulikuwa kunatokea majukumu mengine, unapewa wewe mwanamke kwenda  kuyafanya ambayo yalikuwa yananeokana ni magumu, hasa yale ambayo yanakuwa kuonana na waasi waliopo. Inakuwa ni ngumu kwenda lakini wanakutuma wewe  ambaye unakwenda pale na unaonekana kama mama kama dada, na wanakusikiliza na wakazungumza na wewe na wanakuamini wanajua huwezi kutumia nguvu katika kupata habari kutoka kwao.

Mkutano huo umeandaliwa na Afrika  ya  Kusini na ulitoa fursa kwa walinda amani wanawake kutoka taifa hilo wanaohudumu kwenye kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB, cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO kutoa uzoefu na changamoto zao.

Kikosi hicho cha FIB kina walinda amani kutoka Afrika Kusini, Malawi na Tanzania.