Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nina matumaini na mazungumzo ya jumatano hii kuhusu Syria- Pedersen

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataif kwa Syria, Geir O.pedersen akizungumza na wanahabari. (PIcha ya maktaba)
UN Photo/Evan Schneider
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataif kwa Syria, Geir O.pedersen akizungumza na wanahabari. (PIcha ya maktaba)

Nina matumaini na mazungumzo ya jumatano hii kuhusu Syria- Pedersen

Amani na Usalama

Saa chache kuelekea jumatano ya wiki hii ambapo wajumbe wa Kamati ya Katiba ya Syria watakutana kwa mara ya kwanza mjini Geneva Uswisi kujaribu kukubaliana kuhusu Katiba ya nchi hiyo iliyoghubikwa na vita, Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa Geir O.Pedersen amerelejea wito wake wa kusitisha mapigano nchi nzima na kuachiliwa kwa wafungwa ili kujenga kuaminiana kati ya pande zinazokinzana.

Akizungumza na wanahabari mjini Geneva hii leo Oktoba 28, Pedersen amesema, “tunawasihi kwa nguvu zote, usitishwaji wa mapigano uheshimiwe na kuwa pia tumekuwa tukisihi usitishwaji mapigano kutekelezwa katika nchi nzima.”

Maoni ya Bwana Pedersen yanakuja wiki mbili baada ya uvamizi wa vikosi vya uturuki katika eneo la kaskazini mashariki mwa Syria ambao ulifuatiwa na kuondolewa kwa vikosi vya Marekani katika eneo hilo.

Pedersen amesisitiza umuhimu wa ukweli kwamba mkutano huo unaashiria mara ya kwanza kwamba kukutana kwa wawakilishi kutoka Serikali ya Syria na vikundi vya upinzaji vilivyokuwa na "umiliki" wa mchakato wa kisiasa kunaweza kumaliza zaidi ya miaka nane ya mzozo wa kikatili ambao umewaua maelfu na kuwafurusha ktoka katika makazi yao ndani ya nchi yao na wengine kukimbilia nje ya nchi.

Mjumbe huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kusema kuwa, wakati ni “vigumu kusema itachukua muda gani kuikamilisha kazi”, ilimradi inafanyika, “kwa makusudi makubwa na tunaona maendeleo, na kama mnavyojua nitakuwa nikiripoti kwa Baraza la Usalama, nina matumaini kuwa ndani ya si muda mrefu ujao, tutaona maendeleo halisi katika majadiliano.”