Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa waangazia kuzihifadhi sauti na picha kwa mfumo wa kidijitali ili kuhifadhi historia ya binadamu

Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wakifufua filamu za kihistoria zilizohifadhiwa kwenye maktaba ya kumbukumbu ya chombo hicho. (Picha hii ni ya Novemba 2004)
UN /Mark Garten
Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wakifufua filamu za kihistoria zilizohifadhiwa kwenye maktaba ya kumbukumbu ya chombo hicho. (Picha hii ni ya Novemba 2004)

Umoja wa Mataifa waangazia kuzihifadhi sauti na picha kwa mfumo wa kidijitali ili kuhifadhi historia ya binadamu

Utamaduni na Elimu

Katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya urithi wa sauti na picha, Umoja wa Mataifa unatambua kazi ngumu ya maelfu ya wataalamu wa kuhifadhi nyaraka wakiwemo wakutubi na watunza nyaraka ambao maarifa yao  na kujitolea kwao vinasaidia kuhakikisha kuwa dunia haipotezi historia yake ya filamu za kale, redio na televisheni.

Nyaraka za sauti na picha zina rekodi za historia za karne ya ishiri na karne ya ishini na moja na hivyo kuruhusu wanadamu kuhamisha  urithi kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Hata hivyo kuhamisha picha na sauti za redio ambazo zinanasa maisha yetu yaliyopita ziko katika hatari ya kupotea kupitia kuharibika au kupotea kwasababu teknolojia iliyokuwa inatumika kuzihifadhi imepitwa na wakati.

Kaulimbiu ya mwaka huu inayolenga kufufua  wakati uliopita kupitia picha na sauti, inasifia uzoefu wa wale ambao wamehifadhi urithi wa zamani kwa ajili ya kizazi kijacho.

Kumbukumbu ya dunia

Mnamo mwaka 2005, shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO walikubali kuadhimisha siku hii kila ifikapo tarehe 27 ya mwezi Oktoba ili kuonesha umuhimu wa hatua za haraka za kuhifadhi sauti na picha ambazo ni juhudi zinazoenda sambamba na programu ya kumbukumbu ya dunia ya mnamo mwaka 1992 ambayo  ilieza kuwa kwa kiasi kikubwa makundi ya picha  sauti na picha kote duniani yameathiriwa na matukio mabaya ambayo yameziharibu kama vile vita, wizi, kuparaganyika, usafirishaji haramu na ukosefu wa fedha za kuhifadhi, vitu vyote hivyo vikichangia kutishia utunzaji wa kumbukumbu hizo kwa karne kadhaa.

Kuzibadili kumbukumbu kutoka analogía kwenda mfumo wa dijitali

Kwa kumbukumbu ambazo bado ziko katika hali nzuri, kuzibadili kutoka katika mfumo wa zamani kuelekea katika mfumo wa kidijitali imekuwa ni njia ya kuepuka mmomonyoko na kushindwa kwa miongo kadhaa ya kujaribu kuongeza maisha ya maktaba za sauti na picha.

Mnamo mwaka 2015, UNESCO ilizindua mradi wa kuchangisha fedha ili kuhamisha kumbukumbu za shirika kutoka mfumo wa zamani. Hifadhi ya shirika na makusanyo ya kihistoria ya sauti na picha ina zaidi ya miaka 70 ya mawazo na matendo kwa ajili ya amani na uelewa wa kimataifa ambao umesheni uwanda mpana wa shirika.