Mkutano wa ITU kufungua njia ya mustakabali wa masafa ya mawasiliano ya redio na teknolojia

28 Oktoba 2019

Mkutano wa dunia kuhusu mawasiliano ya redio, mkataba wa kimataifa unaodhibiti masafa adimu ya mawasiliano ya redio na matumizi ya setilaiti umeaanza rasmi hii leo mjini Sharm El-Sheikh nchini Misri.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake kwa njia ya video kwenye mkutano huo wa 19 wa mawasiliano ya Redio duniani WRC-19 amesema “mkutano huu unaofanyika kila baada ya miaka mitatu au minne unawajibika kutathimini na kufanyika mabadiliko kanuni za masuala ya Redio, mkataba wa kimataifa unaosimamia matumizi ya masafa ya redio na njia za obit”.

Naye katibu mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na habari na teknolojia za mawasiliano ITU, Houlin Zhao amesisitiza kuwa, “mkutano huu wa dunia wa mawasiliano ya redio uliofunguliwa leo utashughulikia suala la teknolojia mpya bunifu zinazoongoza hivi sasa duniani ambazo zitakuwa na mchango mkubwa wa katika uchumi wa kesho wa kidijitali  na mustakabali wa maendeleo ya huduma, mifumo na teknolojia.” 

Amesema kwamba ujumuishwaji katika masuala ya kidijitali unatoa fursa za kuboresha maisha ya mamilioni ya watu duniani. “Mabadiliko ya kuunganisha watu na mitandao ya kidijitali yanafanyika yakiwa na changamoto kubwa katika sekta ya mawasiliano na ICT ambayo ni ya matrilioni ya dola katika kusongesha mbele malengo mengo ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo endelevu.”

Katibu Mkuu ameishukuru serikali ya Misri kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kimataifa na kihistoria mjini Sharm El-Sheikh.

Bado kuna wanaosalia nyuma katika zama za kidijitali

“Leo hii mabilioni ya watu na vifaa vya kidijitali wameunganishwa na mtandao wa intaneti na kuongeza ufanisi wa viwanda na makampuni, bado nusu ya watu wa dunia hawajaunganishwa na teknolojia za kisasa” amesema Bwana Mario Maniewicz mkurugenzi wa kituo cha mawasiliano ya Redio cha ITU na kuongeza kuwa, “wakati tukiingia katika zama za kidijitali na mabadiliko ya kimazingira, tunapaswa kuhakikisha kwamba maamuzi yatakayochukuliwa katika WRC-19 sio tu kwamba yatahakikisha na kuruhusu teknolojia mpya na huduma kupelekwa kila mahali bila kuingilia ziliopo ,lakini pia kuhakikisha faida za teknolojia hizo mpya zinamfikia kila raia wa dunia hii, kuleta uweekano wa faida kwa jamii zetu, kwa uchumi wa dunia na mazingira."

UNIFIL
Msimamizi wa mawasiliano wa UNIFIL kutoka Malaysia akiwasiliana kwa kutumia mitambo ya kijeshi akiwa katika majukumu mjini Marakah, Kusini Mashariki mwa Lebanon

 

Binadamu na teknolojia za siku za usoni

Mkutano huo pia utadhihirisha uwezekano mkubwa wa maendeleo ya binadamu na kusongesha malengo mengi ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo endelevu (SDGs).

Utatoa nyenzo kwa ajili ya hatua Madhubuti za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kutoa njia bora kwa ajili ya fursa za huduma za afya, kuboresha kilimo na kupunguza umasikini na njaa, kuboresha nishati salama, kuwezeka mifumo ya usafiri ya intelijensia na mawasiliano miongoni mwa mashine, kuifanya miji kuwa bora na jamii kuwa endelevu. 

Kuhakikisha usafiri salama nchi kavu, angani na majini na kuruhusu nchi kushiriki katika uchumi wa kidijitali kwa kutoa fursa  za watu kuunganisha kwa gharama nafuu na mawasiliano ya brodbandi hususan katika jamii ambazo hadi sasa hazina mawasiliano .

Miongoni mwa ajenda zitakazopewa kipaumbele katika mkutano huo ni kuwezesha ubunifu katika teknolojia mpya za simu za rununu, kubaini masafa kwa ajili ya maendeleo ya baadaye ya muungano wa kimataifa wa mawasiliano ya simu za rununu (IMT) na kuwezesha zaidi uzinduzi wa mitandao ya IMT hapo 2020 ambayo pia juhulikana kama 5G.

Washiriki Zaidi ya 3500 kutoka nchi 193 , wanachama wa ITU wanashiriki katika mkutano huo wa WRC-19, mashirika ya kimataifa pamoja na waangalizi 267 kutoka miongoni mwa wajumbe wa sekta binafsi wa ITU.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud