Milima ni muhimu katika mabadiliko ya tabianchi na mnepo wa majanga:WMO

29 Oktoba 2019

Milima mirefu zaidi duniani kuanzia Andes hadi Alps na ukanda wa milima  Himalaya-Hindu Kush  na Tibet hadi maeneo ya kitropiki imeathirika vibaya na mabadiliko ya tabianchi na athari hizo sasa zinashuka chini kwenye baadhi ya maeneo yenye idadi kubwa ya watu duniani.

Kwa mujibu wa shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO, kuyeyuka haraka kwa theluji milimani kumekuwa chanzo kikubwa cha maji katika mito mingi . Na mito hiyo ni muhimu kwa binadamu, mfumo wa maisha, kilimo, viwanda na pia kutumika kama njia ya usafiri.

Lakini utabiri wa hali ya hewa, mabadiliko ya tabianchi na huduma za udhibiti wa maji mara nyingi havikidhi haja , na hatari kama kuporomoka kwa theluji na maporomoko ya udongo kila mara hupoteza maisha ya watu na kusambaratisha maisha kwa ujumla.

Kwa kulitambua hilo WMO na wadau wengine wameitisha mkutano wa ngazi ya juu wa masuala ya milima kuanzi leo Jumanne Oktoba 29-31, ambao unawaleta pamoja daidi ya wadau 150 kutoka kote duniani.

Lengo la mkutano

Watu hao wanakusanyika kwa lengo la kubaini hatua za vipaumbele ili kusaidia maendeleo endelevu, kupunguza hatari ya majanga na kujenga mnepo wa mabadilikoya tabianchi katika maeneo ya milimani na mabondeni.

Hatua hizo zinajumuisha mkakati wa kuboresha huduma za utabiri wa hali ya hewa katika kushughulikia athari na udhibiti wa rasilimali za maji majanga.

Kwa mujibu wa WMO “Maeneo ya milima yanachukua takribani robo ya ardhi ya dunia na ni maskani ya karibu watu bilioni 1.1. Mara nyingi yanajulikana kama minara ya maji ya dunia kwa sababu mabonde ya mito inayopokea maji kutoka milimani inasambaza maji kwa zaidi ya nusu ya watu wote duniani ikiwemo katika milima ya Himalaya na ukanda wa Tibet unaojulikana kama nchi ya tatu.”

Geir Braathen
Theluji katika milima ya Alps inayeyuka kwa kasi na wataalamu wanakadiria kuwa inaweza kutoweka kufikia mwaka 2100

 

Athari za mabadiliko ya tabianchi

Hata hivyo hivi sasa hatari ni kubwa hasa katika milima yenye vilele virefu kwani ongezeko la joto linaloendelea duniani husababisha theluji na barafu kuendelea kuyeyuka, kutishia uhakika wa chakula, usambazaji wamaji na usafiri kupitia mito.

Vilele maarufu kama vya mlima Everest. Mont Blank, Kilimanjaro na milima Rocky vyote vimeathirika.

Akizungumzia hali halisi katibu mkuu wa WMO Petteri Taalas amesema, “ongezeko la kububujika kwa theluji, kuyeyuka kwa barafu na kutoweka kwa barafu inayofunika milima labda ndio dalili kubwa na dhahiri ya mabadiliko ya tabianchi.Kumekuwa na kuongezeka kuyeyuka kwa theluji katika maeneo 31 yenye barafu duniani hususan katika miongo miwili iliyopita.”

Mkutano huo utamalizika kwa kupitisha wito wa kuchukua hatua za haraka kwenda sanjari na mabadiliko haya yanayofanyika kwa kasi kubwa.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud