Maandamano kila kona ya dunia pengo la kutokuwa na imani lazima lizibwe:Guterres

25 Oktoba 2019

Maandamano yametawala kila kona duniani katika siku za hivi karibuni hali inayoashiria kwamba “watu wana machungu na wanataka kusikilizwa “ na viongozi wao wa kisiasa ambapo ni lazima washughulikie pengo linaloongezeka la kutokuwa na imani, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Oktoba 25 mjini New York Marekani Guterres amesema kwamba ingawa “kila hali ni tofauti na ya kipekee kuna sababu ambazo zinafanana ambazo zinasababisha ongezeko la vitisho katika tofauti za kijamii baina ya raia na wanasiasa. Watu wanataka usawa ukiwemo wa kijamii , kiuchumi, na mifumo ya kifedha ambayo inafanya kazi kwa faida ya wote pamoja na kuheshimu haki zao za binadamu na kuwa na sauti katika maamuzi ambayo yanawaathiri. ”

Maandamano ya hivi karibuni yameshuhudiwa katika mitaa ya Bolivia, Chile, Hong Kong, Equador, Egypt, Guinea, Haiti, Iraq na Lebanon, imesema ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa mapema leo mjini Geneva Uswis. Na maandamano makubwa yaliyoshuhudiwa mapema mwaka huu yalikuwa nchini Algeria, Honduras, Nicaragua, Malawi, Urusi, Sudan, Zimbabwe, Ufaransa, Hispania na Uingereza.

Hakuna sababu inayohalalisha machafuko

Katibu Mkuu Guterres amesema “ametiwa wasiwasi mkubwa kwamba baadhi ya maandamano yamesababisha machafuko na watu kupoteza maisha “Serikali zina wajibu wa kutekeleza haki ya uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani na pia kulinda maeneo ya raia.”

Amesongeza kuwa wakati vikosi vyote vya ulinzi na usalama vinapaswa kujizuia na matumizi yoyote ya nguvu pia na kwa upande wa waandamanaji vilevile , wafuate mfano wa Gandhi, Martin Luther King Jr na vinara wengine wanaopigia upatu mabadiliko yasiyo na machafuko.

“Hakuwezi kuwa na sababu yoyote inayohalalisha machafuko wakati wowote. Zaidi ya hayo natoa wito kwa viongozi kila mahali kusikiliza matatizo halisi ya watu. Dunia yetu inahitaki hatua na dhamira kuweza kujenga utandawazi ulio sawa, kuimarisha uatangamano katika jamii na kukabiliana na hatari za mabadiliko ya tabianchi.”

Guterres amehitimisha kwa kutoa ushauri kwa walioko madarakani “kuanzia nchini Algeria hadi Zimbabwe, kwa mshikamano  na será imara, viongozi wanaweza kuonyesha wanaelewa na kuoongoza njia ya kuelekea kwenye dunia iliyo na haki zaidi.”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter