Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwalimu Tabichi ang'ara tuzo ya Umoja wa Mataifa

Peter Tabichi, mshindi wa tuzo ya mtu wa Umoja wa Mataifa nchini Kenya mwaka 2019 na mshindi wa tuzo ya mwalimu bora duniani 2019.
UN Kenya/ Tirus Wainaina
Peter Tabichi, mshindi wa tuzo ya mtu wa Umoja wa Mataifa nchini Kenya mwaka 2019 na mshindi wa tuzo ya mwalimu bora duniani 2019.

Mwalimu Tabichi ang'ara tuzo ya Umoja wa Mataifa

Masuala ya UM

Mwalimu Peter Tabichi ambaye amepata umaarufu mkubwa  baada ya kutunukiwa tuzo ya mwalimu bora duniani mwaka 2019 , sasa ameibuka kidedea tena na kuwa mshindi wa tuzo ya mtu bora kwa Umoja wa Mataifa nchini Kenya mwaka huu. Tuzo ambayo hutolewa nchini humo kwa mtu ambaye ameleta mabadiliko chanya katika jamii yake.

Akizungumza na kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa UNIC jijini Nairobi Kenya pindi tu baada ya kupokea tuzo hiyo Alhamisi, Bwana Tabichi ameelezea maana ya tuzo hiyo kwake ambapo amesema, "hili tuzo ambalo nimepewa, ni tuzo muhimu kabisa, kwa Maisha yangu. Na sio tu kwa maisha yangu mimi, pekee yangu, pia kwa maisha ya wengine. Kuna watu wengi katika jamii wanafanya mambo mengi mazuri, kwa hivyo kupewa hili tuzo sio kwamba mimi ni bora kuwaliko, ni kuashiria zile kazi Nzuri ambazo hawa watu wanafanya katika jamii. Kwa hivyo, ninachukua muda huu kuwashukuru haswa wanafunzi wangu ambao wameweza kufanya mambo mengi mazuri. Wameweza kufanya mambo mengi ambayo ni mazuri ambayo yameniwezesha mimi pia kutambulika. Na pia ningeshukuru walimu wenzangu ambao tunafanya kazi pamoja na wao. Kwa hivyo ninaweza sema kwamba tumeshirikiana. Huo ushirikiano ndio umeweza kunisaidia kutambulika. Kwa hivyo, niseme kwamba hii ni muhimu kabisa Kwangu Na pia kwa wengine. Kwa hivyo nashukuru Mungu , nashukuru wengine pia."

Ama kweli mafanikio ya mtoto ni juhudi za mzazi  na baba yake mzazi Lawrence Tabichi  hakuficha furaha yake akisema, "nilisikia furaha kubwa, hata sikuamini ni yeye. Kwa hivyo , niliweza kushuhudia kweli ni yeye? Kwa hivyo nilifurahi. Nilimkumbatia huyu kijana wangu, mvulana huyu wangu, ninamwona kama ni fahari Kwa watoto wangu. Anaonyesha talanta nyingi zaidi kuliko wengine. Kwa sababu, alianza wakati alikuwa bado mchanga. Tena elimu yake kutoka msingi hadi chuo kikuu, alifanya vyema. Alinifanya nijisikie mzazi bora kwake".