Hofu ya njia za uzazi wa mpango yasababisha wanawake kubeba ujauzito usiopangwa- WHO

Uzazi wa mpango
UNFPA
Uzazi wa mpango

Hofu ya njia za uzazi wa mpango yasababisha wanawake kubeba ujauzito usiopangwa- WHO

Afya

Utafiti mpya wa shirika la afya ulimwenguni, WHO, umebaini kuwa theluthi mbili ya wanawake wenye uwezo wa kubeba mimba na ambao wana nia ya kuchelewesha kupata ujauzito au kudhibiti idadi ya watoto huacha kutumia huduma za uzazi wa mpango kwa hofu ya madhara ya huduma hizo.

Taarifa ya WHO iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi inasema kuwa matokeo  hayo ni kutokana na utafiti katika nchi 36 na kwamba wanawake hao kutokana na hofu hizo hatimaye wanajikuta na ujauzito usiotarajiwa.

WHO imesema wanawake hao wanahofia kuwa wakitumia huduma za uzazi wa mpango wanaweza kupata athari za kiafya pamoja na kutoweza kupata ujauzito baadaye.

Shirika hilo linasema ingawa mimba zisizopangwa si lazima ziwe mimba zisizohitajika, bado zinaweza kusaababisha madhara ya kiafya kwa mama na mtoto kama vile utapiamlo, magonjwa, ukatili, kupuuzwa na hata kifo.

“Mimba zisizopangwa zinaweza kusababisha pia kiwango kikubwa cha kuwa na watoto wengi, kiwango kidogo cha elimu, ukosefu wa ajira na  umaskini, changamoto ambazo zinaweza kukumba kizazi na kizazi,” imesema taarifa hiyo ya WHO.

Muarobaini ni huduma bora zaidi za uzazi wa mpango

WHO inasema njia za uzazi wa mpango ni muhimu katika kuzuia mimba zisizopangwa na tafiti zinaoyesha kuwa, “asilimia 85 ya wanawake walioacha kutumia njia hizo wamepata ujauzito katika miaka ya mwanzo. Miongoni mwao waliokumbwa na mimba zisizotarajiwa na kuamua kuzitoa, waliacha kutumia njia za uzazi wa mpango kwa hofu ya afya zao, madhara ya njia hizo na changamoto za matumizi.”

 Akizungumzia ripoti hiyo, Dkt. Mari Nagai kutoka WHO amesema, shaka na shuku hizo zinaweza kushughulikiwa kupitia ushauri nasaha bora kuhusu huduma za uzazi wa mpango na usaidizi kwa wanaotaka kuzitumia njia hizo.


Mapendekezo

Utafiti huo unapendekeza mwelekeo unaolenga mbinu za uzazi wa mpango zinazoendana na mahitaji na matakwa ya mtumiaji, kubaini mapema wakati wanawake na wasichana wana hofu kuhusu njia ya uzazi wa mpango wanayotumia na kuwezesha wanawake na wasichana kubadili mbinu za uzazi wa mpango huku wakipatiwa ushauri nasaha.

Takwimu zinaonesha kuwa duniani kote wanawake milioni 74 wanaoishi kwenye nchi za kipato cha kati na chini kila mwaka hupata mimba zisizotarajiwa.

WHO inasema hali hiyo inasababisha milioni 25 kutoa ujauzito kwa njia zisizo salama hali inayosababisha vifo 47,000 kila mwaka.