Dola milioni 89.5 zahitajika kuwezesha Zambia kujikwamua na janga la kibinadamu- OCHA

25 Oktoba 2019

Nchini Zambia, Umoja wa Mataifa na wadau wake wamezindua ombi la dola milioni 89.5 kusaidia nchi hiyo kukabiliana na janga la kibinadamu kwa miezi saba ijayo, janga ambalo limesababishwa na msimu mbaya wa mvua unaokumba taifa hilo tangu mwaka 1981 hususan kusini mwa nchi hiyo.

Msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Jens Laerke ameaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo kuwa uhaba wa mvua umekwamisha uzalishaji wa chakula, mathalani uzalishaji wa mahindi ambalo ni chakula kikuu cha taifa hilo umepungua kwa asilimia 16.

Bwana Jens amesema, kuporomoka kwa uzalishaji wa mahindi umesababisha taifa hilo ambalo awali lilikuwa linauza mahindi nje ya nchi, lipige marufuku biashara ya mahindi nje ya nchi huku pia magonjwa ya mifugo yakisakama taifa hilo.

Ameongeza kuwa zaidi ya watu milioni 2.4 kati ya jumla ya watu milioni 17 wa taifa hilo wanatarajiwa kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula wakati wa msimu wa mwambo kuanzia mwezi huu wa Oktoba hadi mwezi Machi mwakani.

“Tathmini yam waka 2019 ya watu walio hatarini imebaini pia ongezeko la viwango vya utapiamlo uliokithiri. Utapiamlo uliokithiri ambao husababisha watoto kudumaa umefikia kiwango cha asilimia 6 kwenye majimbo 9 ya Zambia. Kiwango cha juu zaidi kimepatikana katika wilya za jimbo la Magharibi. ikiwemo Shang’ombo, Sioma na Kalabo.

Amesema ni kwa kuzingatia hilo, Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia ya kimataifa wanasaka jumla ya dola milioni 89.5 ili kutoa misaada ya dharura ya kibinadamu kwa watu milioni 2.3 kwa kipindi cha miezi 7 ijayo.

“Idadi kubwa ya fedha hizi itatumika kwenye msaada wa chakula. Ombi hili linalenga kuunga mkono mpango wa serikali wa kujikwamua ambao unasaka kupatia huduma za kujikwamua watu milioni 2.3 katika miezi 12 ijayo,”  amesema Bwana Laerke.

Amesema kuwa serikali tayari imechangisha dola milioni 36.7 kwa ajili ya kuhakikisha watu wana uhakika wa chakula, lishe, huduma za afya na za kujisafi, usalama na elimu lakini hata hivyo serikali hiyo ya Zambia imeomba wadau wa kimataifa wasaidie kuziba pengo la ufadhili lililopo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter