Kuelekea UN75, kampeni yaanzishwa kuhoji wananchi mustakabali wautakao

24 Oktoba 2019

Kuelekea maadhimisho ya miaka 75 ya Umoja wa Mataifa mwakani 2020, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres hii leo ametangaza kuwa maadhimisho hayo yatajumuisha mjadala jumuishi wa dhima ya jukumu la ushirikiano wa kimataifa katika kujenga mustakabali  utakiwao ulimwenguni.

Kauli hiyo ya Guterres imo kwenye video iliyotolewa hii leo katika maadhimisho ya miaka 74 ya chombo hicho chenye wanachama 193 na tayari kuna ukurasa maalum wa kuelekea maadhimisho hayo na mtu anaweza kujiunga na mjadala.

Kuanzia mwezi Januari mwaka 2020, Umoja wa Mataifa utakuwa na mijadala duniani kote ukivuka mipaka na ukihusisha vizazi tofauti. Lengo ni kufikia umma, kusikiliza matumaini na hofu zao na kujifunza kupitia uzoefu wao,” amesema Katibu Mkuu.

Umoja wa Mataifa ulianzishwa mwaka 1945, kusaidia juhudi za pamoja za kufikia amani, maendeleo na haki za binadamu kwa wote ambapo, “kampeni  ya UN75 inasaka kuibua mjadala na hatua za jinsi tunaweza kuwa na dunia bora zaidi licha ya changamoto tunazokabiliana nazo,” amesema Katibu Mkuu.

Guterres amesema ingawa kampeni hiyo ya UN75 inalenga kuchochea mjadala katika ngazi mbalimbali za kijamii- kuanzia madarasani hadi vyumba vya mikutano, bungeni hadi vijijini- itaweka msisitizo zaidi kwa vijana na wale ambao sauti zao mara nyingi huwa zinaenguliwa au hazisikiki katika masuala ya kimataifa.

Natoa wito kwa kila mtu popote alipo, apaze sauti yake kwenye kampeni hii: Tunataka kusikia maoni yenu, mikakati yenu, mawazo yenu ili sisi tuweze kutoa huduma bora zaidi kwa watu tunaowahudumia,” amesisitiza Katibu Mkuu.

Kupitia mijadala hiyo, kampeni ya UN75 inalenga kujenga dira ya dunia kwa mwaka 2045, ambayo itakuwa miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa lengo likiwa ni kuongeza uelewa wa vitisho kwa siku za usoni na kuchochea hatua za pamoja kufanikisha dira hiyo.

Umoja wa Mataifa  unasema katika kampeni hiyo, kura za maoni na uchambuzi kupitia vyombo vya habari  utafanyika sambamba na kupata takwimu sahihi na wakilishi.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, maoni na mawazo yatakayopatikana kupitia kampeni hiyo yatawasilishwa kwa viongozi wa dunia na maafisa waandamizi wa Umoja wa Mataifa kwenye kikao cha ngazi ya juu wakati wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba mwakani, sambamba na kusambazwa kupitia mitandao ya kijamii na wadau.

Umoja wa Mataifa umesisitiza kuwa hakuna ukomo au masharti ya kushiriki kampeni hiyo iwe kwa kushiriki moja kwa moja au kupitia mtandao.

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter