Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa WFP akutana na viongozi wa Sudan huko Khartoum

Mgao wa chakula huko Pieri nchini Sudan Kusini ambako WFP inasaidia watu 29,000 kati yao 6,600 ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano. (Picha 5 Februari 2019)
WFP/Gabriela Vivacqua
Mgao wa chakula huko Pieri nchini Sudan Kusini ambako WFP inasaidia watu 29,000 kati yao 6,600 ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano. (Picha 5 Februari 2019)

Mkuu wa WFP akutana na viongozi wa Sudan huko Khartoum

Msaada wa Kibinadamu

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la mpango wa chakula duniani, WFP David Beasley amehitimisha ziara ya siku mbili nchini Sudan ambako alikutana na viongozi wa serikali mpya sambamba na kutembelea eneo la Kosti ambako alizindua msafara mmoja kati ya mitatu ya usafirishaji wa chakula cha msaada kuelekea Sudan Kusini.

Shehena hizo zinasafirishwa kwa njia ya maji kupitia mto Nile na ni msafara wa kwanza tangu mwaka 2011.

Taarifa ya WFP iliyotolewa leo mjini Khartoum nchini Sudan imemnukuu Bwana Beasley akisema kuwa, “hii ni zama mpya kwa Sudan, Sudan ambayo inaweza kuwa na athari chanya kwa mustakabali wa eneo zima.”

Kauli hiyo ya Mkuu huyo wa WFP ameitoa  baada ya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok akiongeza kuwa, “WFP imekuwa mdau wa muda mrefu wa wananchi wa Sudan na tuko tayari kuendelea kusaidia serikali na wananchi wake katika kipindi hiki cha kihistoria.”

 Wakati wa ziara yake huko Kosti, Beasley alishuhudia meli tatu zinazolipwa na WFP zikipakia tani 4,5000 za chakula kilichozalishwa Sudan na kisha meli hizo zilisafiri kupitia mto Nile hadi kwenye miji ya Renk, Malakal na Bor nchini Sudan Kusini.

WFP inasema shehena hizo zitakidhi mahitaji ya watu 370,000 wa Sudan Kusini kwa mwezi mmoja.

Usafirishajiwa shehena za kibinadamu kwa  njia ya mto kutoka Sudan hadi Sudan Kusini ulikoma kwa kiasi kikubwa baada ya uhuru wa Sudan Kusini mwaka 2011.

Kurejea kwa njia hii ya usafirishaji unafuatia ushirikiano kati ya serikali za Sudan na Sudan Kusini na kwa kutambua kwa pande mbili hizo umuhimu wa usafirishaji wa bidhaa za misaada kwenye maeneo yaliyokumbwa na mzozo huko Sudan Kusini.

Kwa mujibu wa WFP, usafirishaji kwa njia ya mto Nile ni gharama nafuu na inatoa mbadala wa usafirishaji kati ya nchi mbili hizo hususan wakati wa msimu wa mvua pindi barabara zinapokuwa zimeharibika.

Tangu mwaka 2014, WFP imesambaza tani 265,000 za msaada wa chakula nchini Sudan Kusini na shehena hizo zilisafirishwa kupitia mipakani.

Hii ni ziara yay a pili ya Mkurugenzi Mtendaji huyo wa WFP nchini  Sudan tangu ashike wadhifa huo mwezi Aprili mwaka 2017.

Wakati wa ziara hiyo alikutana pia na mwenyekiti wa Baraza la Utawala la Sudan Luteni Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan, Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo, Luteni Jenerali Mohamed Hamdan Hemeti na Mawaziri wa Kigeni, Kilimo, Kazi na Maendeleo ya  Jamii pamoja na Naibu Waziri wa Fedha ambako walijadili kipindi cha kihistoria cha mpito Sudan na umuhimu wa kupanua wigo wa utoaji wa misaada ya kibinadamu nchini humo.