Mkataba wa WHO na IGBA utaimarisha upatikanaji wa dawa na hatimaye afya kwa wote:WHO

22 Oktoba 2019

Shirika la afya Ulimwenguni, WHO limetia saini leo Jumanne makubaliano na taasisi ya kimataifa ya dawa zinazotengenezwa bila kufuata masharti ya ataza ambayo ni haki ya umiliki wa dawa halisi, IGBA kwa ajili ya kuimarisha upatikanaji wa dawa kwa wote ambao hukwamishwa na sababu mbali mbali.

WHO kupitia taarifa yake imesema vikwazo vikubwa na bei za juu pia maswala ya usimamizi kwa mfano msururu katika kuleta dawa kwenye soko ni miongoni mwa changamoto ambapo katika kukabiliana na changamoto hizo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus na mwenyekiti wa IGBA Jim Keon wamefikia makubaliano hayo kama sehemu muhimu ya WHO kuhakikisha huduma ya afya kwa wote kwa kutambua umuhimu wa dawa zinazotengenezwa bila kufuata masharti ya ataza ambayo ni haki ya umiliki wa dawa halisi, kwa ajili ya kuhakikisha tiba inapatikana kwa wote na kwa bei nafuu.

WHO inaunga mkono matumizi ya dawa za hizo huku idadi kubwa ya bidhaa katika orodha ya WHO ya dawa muhimu ni dawa zinazotengenezwa bila kufuata masharti ya ataza.

Programu ya WHO ambayo hupitisha viwango vya dawa zinazowasilishwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika mengine katika nchi za kipato cha chini imetoa kipaumbele katika matumizi ya dawa za hizo kama njia ya kutibu watu wengi kwa raslimali zilizopo huku asilimia 70 ya dawa zikitajwa kama dawa zinazotengenezwa bila kufuata masharti ya ataza.

Mkataba huo mpya kati ya WHO na IGBA umeashiria nafasi ya sekta ya dawa katika kusaidia WHO kuweka vifaa vya kuwezesha usajili wa dawa zinazotengenezwa bila kufuata masharti ya ataza na utasaidia katika kupunguza mzigo wa majaribio ya kliniki, kuharakisha usajili na kuimarisha upatikanaji.

Ushirikiano huo ni hatua ya kwanza muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya na dawa kwa muda mrefu kwa ajili ya hatua kuelekea huduma ya afya kwa wote ifikapo 2030.

WHO kwa sasa kwa mujibu wa utafiti huru inaokoa dola milioni 590 duniani kila mwaka ambazo zinetumika kutengeneza dawa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud