Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto mizozoni wako hatarini kutokana na pengo la ufadhili-UNICEF

Watoto nchini Jamhuri ya kidemkrasia ya Congo,DRC
© UNICEF/Vincent Tremeau
Watoto nchini Jamhuri ya kidemkrasia ya Congo,DRC

Watoto mizozoni wako hatarini kutokana na pengo la ufadhili-UNICEF

Haki za binadamu

Mamilioni ya watoto katika maeneo yalioathiriwa na majanga ya asili na yale yenye mizozo wako hatarini kutokana na ukata wa ufadhili kwa miradi ya misaada ya kibinadamu ya kuokoa maisha. Limesema Shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF.

Kulingana na taarifa iliotolewa na UNICEF hii leo mjini New York Marekani kuna pengo la aslimia 46 la ufadhili wake wa mwaka 2019 wa dola bilioni 4.16, sasa ikaribia robo ya mwisho wa mwaka.

Fedha hizo zilikuwa zishughulikie mahitaji ya msingi ya afya, elimu, lishe na ulinzi kwa watoto milioni 41 katika  nchi 59 mwaka huu.

Hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore amesema mamilioni ya watoto walio hatarini duniani wanazidi kuwa wahanga wa madhila ya mzozo wa kibinadamu.

Pia anasikitika kutaja kwamba bila msaada wa ziada, watoto hao hawatahudhuria shule wala kuchanjwa, kupata lishe sitahili au kulindwa dhidi ya ukatili na unyanyasaji.

Fore ameongeza kuwa, wakati ambapo wanaendelea kuzitolea wito pande husika kukomesha mizozo na dunia kujiandaa zaidi kwa masuala ya dharura, hawawezi kusahau kurejelea ombi la msaada wa ziada wa kibinadamu kutoka kwa wahisani, ili kukidhi mahitaji ya msingi wa watoto hawa.

Mkurugenzi Mtendaji huyu wa UNICEF, ametaja baadhi ya nchi zinazokumbwa na pengo kubwa zaidi la ufadhini kuwa ni Pakistan, Cameroon, Burkina Faso na Venezuela.

Mahitaji ya dharura katika mizozo ya muda mrefu nchini Syria na majirani zake, Yemen, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Bangladesh pia yamesalia na pengo kubwa la ufadhili.

 UNICEF imesema ikiwa ukata utaendelea hadi mwishoni mwa mwaka huu madhara yake kwa watoto yatakuwa makubwa zaidi.