Kuishi maisha ya kawaida ukiwa na VVU inawezekana:Evelyn

22 Oktoba 2019

Kuwa na virusi vya HIV au VVU sio hukumu ya kifo tena na unaweza kuishi maisha ya kawaida na kulewa watoto wako, anasema Evelyn kutoka Kenya ambaye amekuwa akishi na VVU kwa muda mrefu sasa huku akilea watoto wake wawili. 

Nairobi Kenya Evelyn ambaye mwanaye wa kwanza alizaliwa na VVU ilikuwa vigumu kwake kwa  miaka mingi kukubali hali yake . Yeye pamoja na mwanaye mwenye VVU pia walikuwa wagonjwa sana, “daktari aliniambia nina miaka mitano tu ya kuishi . Na wakati nilipoanza kutumia dawa za kupunguza makali ya UKIMWI baada ya kujaribu kila njia , mizizi, sala , hakuna hata moja iliyofanya miujiza kwangu kama ARVs”.

Lakini kupitia dawa hizo anazokunywa zinazotolewa kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na UKIMWI, UNAIDS, maisha ya Evelyn yalibadilika mwaka 2011, na ndoto yake ya kuwa na watoto zaidi ikatimia,“nilikwenda kufanyiwa vipimo tena na virusi havikuonekana, daktari akanishauri kama unataka kupata mtoto mwingine sasa unaweza. Hivyo nikafikiria ninaweza kuwa kwenye mahusiano? Ndio unaweza kuishi maisha ya kawaida, sikuwa na imani mpaka nilipojaribu”

Na mwanaye wa pili alizaliwa bila VVU, “ni fahari kubwa kwangu, ni furaha yangu kubwa , na nakuhakikishia iko katika kila moyo wa mama mwenye VVU”

Wanawake kama Evelyn ni takriban nusu ya watu wote wanaoshi na VVU  Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara. Hivi sasa Evelyn anahamasisha wanawake wengine katika makundi na pia kutumia kipindi chake cha Redio kusambaza ujumbe na kuelimisha,“na inaanza na mimi na inaanza na wewe, kila mmoja fanya vipimo na ukikutwa nao pata matibabu”

Kwa mujibu wa UNAIDS leo hii zaidi ya watu milioni 23 wanapata ARVs kote duniani, yakiwa ni mafanikio makubwa katika kuelekea kutokomeza UKIMWI.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud