Kila jambo ambalo wanawake wameweka mkono wao, limeonesha mafanikio- Amina J. Mohammed

21 Oktoba 2019

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi. Amina J. Mohammed hii leo akiwa ziarani mjini Addis Ababa nchini Ethiopia amelihutubia Baraza la Amani na Usalama la Muungano wa Afrika, AU,  na kuupongeza Muungano huo kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi yao ya kuhakikisha usawa wa kijinsia na ushiriki wa wanawake.

“Hili ni eneo jingine ambalo tuna malengo sawa ya pamoja. Katibu Mkuu amejitolea sana kwa uongozi wa wanawake na ushiriki wa kisiasa kama sehemu ya maono yake ya kuzuia migogoro.” Amesema Bi Mohammed.

Bi Mohamed ameongeza kuna uthibitisho mkubwa kwamba ushiriki wa wanawake hufanya michakato ya amani na usalama kuwa jumuishi zaidi, yenye ufanisi na ya kudumu.

Aidha ametoa mifamo ya namna mbalimbali wanawake wanavyohusika katika masuala ya kijamii na walivyo muhimili mkubwa katika kuleta amani na usalama akisema katika maeneo ambayo kumekuwa na migogoro, upatanisishi unaosimamiwa na wanawake umeonesha mafanikio.

“Zaidi ya hayo, tunajua kuwa uongozi wa wanawake katika michakato ya kufanya maamuzi ya kisiasa unaboresha matokeo kwa kila mtu katika jamii.” Ameongeza Bi Mohamed

Vilevile ameeleza kuwa katika ulinzi wa amani, mahali ambako Umoja wa Mataifa una walinzi wa amani wanawake wanajeshi na wale wanaohudumu kama raia, matokeo ni makubwa.

Hata hivyo Bi Mohamed amesema takwimu zinabaki kuwa zenye kuleta wasiwasi mkubwa kwani Wanawake ni asilimia 4 tu ya walinda amani wa vikosi vya Umoja wa Mataifa.

Akitoa takwimu za athari za mifarakano inavyowaathiri wanawake Bi Mohammed amesema mathalani mwaka jana ulishuhudia viwango vya juu vya dhuluma za kisiasa kulenga wanawake. Mtu mmoja kati ya wanawake 5 waliofurushwa, hukumbana na dhuluma ya kijinsia na nchi 9 kati ya 10 zilizo na viwango vya juu vya ndoa za watoto ziko katika hali mbaya.

“Katika siku zijazo, tutasafiri kwenda Djibouti, Somalia, na Eritrea kwa lengo la amani ya Wanawake na Usalama na maendeleo. Huu ni ujumbe wa tatu wa pamoja wa Muungano wa Afrika na Muungano wa Ulaya. Katika miaka iliyopita, tumetembelea DRC, Nigeria, Sudani Kusini, Niger na Chad.” Amesema.

Aidha Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akihutubia mkutano mwingine kuhusu jukumu la wanawake katika kushughulikia biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu, ameanza kwa kuipongeza Ethiopia kwa kuonesha uongozi katika mapambano dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu, ikiwa ni nchi ya kwanza ya kusini mwa jangwa la Sahara kuungana n anchi nyingine 30 kuunga mkono kampeni ya Umoja wa Mataifa ifahamikayo kama Blue Heart Campaign yaani Moyo wa Buluu.

“Nchi pia imekuwa kiongozi katika kukuza ushiriki wa wanawake katika maisha ya umma, pamoja na baraza la mawaziri la kisiasa ambalo nusu ni wanawake. Kwa kweli, Tuzo ya Amani ya Nobel iliyotolewa hivi karibuni kwa tu kwa Waziri Mkuu Abiy Ahmed ilionyesha jukumu lake katika "kuongeza sana ushawishi wa wanawake katika maisha ya kisiasa na ya kijamii ya Ethiopia." Amepongeza Bi Mohammed.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter