Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya hatari wahamiaji kutoka Afrika kuelekea Ulaya watafunga safari hizo tena-Ripoti UNDP

Wahamiaji wawili vijana kutoka Gambia wakiangalia ramani baada ya kuvuka Italia mwaka 2016.(Maktaba)
© UNICEF/Ashley Gilbertson
Wahamiaji wawili vijana kutoka Gambia wakiangalia ramani baada ya kuvuka Italia mwaka 2016.(Maktaba)

Licha ya hatari wahamiaji kutoka Afrika kuelekea Ulaya watafunga safari hizo tena-Ripoti UNDP

Wahamiaji na Wakimbizi

Wahamiaji wasio wa kawaida waliofunga safari hatarishi kutoka bara Afrika hadi Ulaya wanaweza kufunga safari hizo tena licha ya kujua hatari za safari hizo imesema ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP leo Jumatatu Oktoba 21.

Kwa mujibu wa ripoti takriban asilimia 93 ya wakimbizi 2,000 wasio wa kawaida waliohojiwa wameelezea kukumbwa na hatari wakati wa safari zao, lakini ni asilimia 2 tu walisema hatari za safari hizo zingewasababisha kusalia nyumbani.

Ripoti hiyo ya UNDP ikipewa jina kupanda milima: Sauti ya wahamiaji wasio wa kawaida kutoka Afrika hadi Ulaya, kwa jili ya kuziba pengo la kimatifa na kutoa picha halisi ya wapi wahamiaji wasio wa kawaida huenda kutoka Afrika hadi Ulaya.

Ripoti imetathmini wahamiaji 1,970 kutoka nchi 39 za Afrika walioko katika mataifa 13 ya Ulaya, ambao wote wamesema kwamba waliwasili Ulaya kwa njia zisizo za kawaida na sio kwa jaili ya kuomba hifadhi au ulinzi kama inavyodhaniwa.

UNDP imetanabaisha kwamba kusaka ajira sio kichocheo pekee cha kuhama na kwamba sio wahamiaji wote wasio wa kawaida ni masikini Afrika, au wanaviwango vya chini vya elimu huku ripoti ikionesha kuwa asilimia 58 ya wahamiaji ama walikuwa wameajiriwa au walikuwa shuleni wakati walipofunga safari zao, huku wengi wakipata kipato cha juu. Hatahivyo asilimia 50 ya waliokuwa wakifanya kazi wamesema hawakuwa wanapata mshahara wa kutosha

Kwa mujibu wa ripoti, “uhamiaji huo unatokana na ari na matamanio ya watu ambao licha ya kuwepo maendeleo barani Afrika lakini hayatimizi ndoto zao. Aidha vikwazo katika kufikia fursa au kukosa chaguo ni moja ya sababu zinazopelekea vijana kuchukua safari hizo”,  amesema Mkuu wa UNDP, Achim Steiner.

Akiongeza kuwa, “kwa kuangazia sababu za watu kuhama kupitia njia zisizo za kawaida na kile wanachokumbana nacho katika safari hizo, ripoti inachangia katika mjadala muhimu wa nafasi ya uhamiji katika hatua kuelekea malengo ya maendeleo endelevu na mbinu bora za kuisimamia.”

Sauti za wahamiaji

Uhamiaji unachukua sura mbili ya wahamaiji wenyewe na familia zao, mfano wa baadhi ya watu waliohojiwa kupitia video ya UNDP ni Hawa Sankareh kutoka Gambia ambaye ni mama wa kijana Mahamadou alioko Italia ambaye amesema,“hii ni nyumba yetu, nyumba ya familia yetu lakini hatuna chochote hapa iwapo Mamadou asingefunga safari kwenda Italia. Kila kitu iwe matibabu au changamoto nyingine yeyote tunamtegemea yeye.”

Kwa upande wake Mahamadou ambaye anaonekana akiwa mjini Roma, Italia anasema,“niliwasili kutoka Gambia niliondoka nchini mwangu Desemba 2013, nikawasili Italia Januari 2014, kabla ya kupata stakabadhi za Italia ni lazima uwaeleze sababu ya kuondoka nchini mwako, niliwaambia iwapo watanisaidia kupata shule nzuri, na wakati nitajifunza kiitaliano nitawasaidia kuwa mtafsiri, kwa ajili ya watu wasio na makazi na wakimbizi ambao wanaishi Ulaya ili waweze kueleweka, ninaweza kusaidia.”

Na pindi mtu anapohamia nchi ya kigeni hali inakuwaje? Julius Myenyini ni mhamiaji kutoka Cameroon ambaye anaishi nchini Sweden,“sasa inakuja changamoto ya kujumuika katika jamii, kukubalika na jamii, nakumbuka nilikuwa na mazungumzo na afisa wa uhamiaji akinielezea kuhusu hali ilivyo Sweden. Mchakato na wapi sehemu ya kupata nini, tarifa nyingi sana lakini unweza kuwa ndani ya jamii na ukakosa kuunganika na jamii hio. Unaweza kuwa na mtu ambaye anazungumza kiswidi safi, ambaye ana ajira lakini hayuko ndani ya jamii ya Sweden. Kwa sababu iwapo mkinijumuisha kama mmoja wenu na sehemu ya jamii nitaihisi nitakuwa na furaha.”

UNDP imesema sababu kuu ya watu kusalia nchi za kigeni ni kwamba hawatumi fedha za kutosha nyumbani na hivyo wanasalia Ulaya. Ripoti inasema asilimia 53 ya wahamiaji walikuwa wamepokea msaada kutoka kwa familia na marafiki ili kuchukua safari hizo na pindi walipowasili Ulaya aslimia 78 walikuwa wanatuma fedha nyumbani. Aidha ripoti imetanabaisha kwamba kuna tofauti kati ya yanayowakumba wanawake na wanaume na tofauti ya kipato barani Afrika ambapo wanaume wanapata ujira bora kuliko wanawake inabadilika pindi wanapowasili Ulaya huku wanawake wakipata asilimia 11 zaidi ya wanaume. Pia idadi kubwa ya wanawake hutuma fedha nyumbani hata wasio na ajira.

Hatahivyo, wanawake ni waathirika wakubwa wa uhalifu huku wengi wakihusika nai uhalifu katika miezi sita ya kwanza kabla ya kuhojiwa na idara ya uhamiaji na wakikabiliwa na ukatili wa kiongono

UNDP imesema ripoti naonyesha dhairi kwamba fursa na chaguo vinahitajika barani Afrika ili kusonga kutoka uhamiaji uliosimamiwa na sio holea ili kuendana na mkataba wa uhamiaji salama na utaratibu.