Mafuriko maeneo ya wakimbizi Sudan Kusini yatishia huduma muhimu ikiwemo afya-UNHCR

18 Oktoba 2019

Mafuriko yasiyotarajiwa yameathiri takriban watu 200,000 kaunti ya Maban nchini Sudan Kusini, ikiwemo wakimbizi na jamii zinazowahifadhi limesema hii leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi, msemaji wa UNHCR, Andrej Mahecic amesema eneo hilo liko katika jimbo la Upper Nile na ni makazi ya zaidi ya wakimbizi 150,000 kutoka Sudan ambako UNHCR na wadau wengine wanahaha kuwasilisha misaada ya dharura wakati huu ambapo watu wanasaka maeneo salama ya nchi kavu.Eneo hilo karibu na mjii mkuu wa Maban wa Buni liko hatarini ya kukumbwa na mafuriko msimu huu wa mvua kubwa. Hatahivyo, kufurika kwa mito nchini Sudan Kuisni ni kutokana na mvua kubwa zinazoshuhudiwa nchi jirani ya Ethiopia.

UNHCR imesema wenyeji wana mahitaji ya dharura kwani wengi wamekimbia makwao huku wakibeba vitu kidogo tu. Aidha mvua hizo zimesababisha mafuriko barabarani kuelekea kambini, shule  zimefungwa, huduma za umma ikiwemo hospitali na huduma za kujisafi  hali ambayo inahatarisha afya.

Bwana Mahecic amesema, “makazi ya muda, maji na huduma za kujisafi zinasalia kuwa mahitaji ya muhimu kwa ajili ya wakimbizi na wenyeji. Kama namna ya kukabiliana na hali, UNHCR imeweka mifuko ya dharura na vifaa vya kusaidia saisi ya familia 5,000, watu 25,000 kujenga na kukarabati makazi yao yaliyoharibiwa, lakini msaada Zaidi unahitajika.”

Kwa sasa Sudan Kusini inahifadhi takriban wakimbizi 300,000 kutoka eneo la Blue Nile na Kordofan Kusini. Zaidi ya watu milioni 1.5 ni wakimbizi wa ndani nchini.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud