Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko kaskazini-mashariki mwa Syria ni "mwiba" kwa wenye ulemavu

Khadijah Mohammad - Um Ismail mkimbizi aliyefurushwa Syria kufuatia mapigano na mwanae, Mustafa ambaye anahitaji kitimwendo  kwa usafiri.
WFP
Khadijah Mohammad - Um Ismail mkimbizi aliyefurushwa Syria kufuatia mapigano na mwanae, Mustafa ambaye anahitaji kitimwendo kwa usafiri.

Machafuko kaskazini-mashariki mwa Syria ni "mwiba" kwa wenye ulemavu

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP linasikitishwa sana na usalama wa raia walioko katika miji ya RAqqa na Hasake kaskazini-mashariki mwa Syria ambako operesheni za kijeshi zinaendeshwa tangu tarehe 9 mwezi huu wa Oktoba.

Video ya WFP inaonesha watu waliofurushwa makwao wakiwa nje ya shule iliyogeuzwa kuwa makazi, tunakutana na Khadijah Mohammd- UM Ismail, akiwa anamsukuma mwanae wa kiume, Mustafa kwenye kiti mwendo, mkononi Mustafa ameshika dawa.

Bi. Khadijah, mjane alikuwa ndio amemaliza kuandaa chakula kwa ajili ya familia yake wakati mashambulizi yalipoanza huku akilazimika kukimbia bila chochote huku akimsukuma mwanae kwa kitimwendo.

(Sauti ya Khadijah) 

“Ilituchukua takriban saa nne barabarani, tulikuwa tunatembea na ilikuwa safari ndefu. Ilichosha sana. Kusukuma kitimwendo cha Mustafa mpaka tulipowasili. Kitimwendo kilikuwa karibu kuharibika wakati tuliwasili.”

Kuna takriban watu 160,000 wanaokimbia kusaka hifadhi miji ya Hasakeh na Raqqa, watu wengi wakiamua kuishi na familia na marafiki badala ya makazi ya pamoja kwa hiyo huenda idadi ni kubwa zaidi. Thalja Modhi ni mkimbizi kutoka Ras al Ain

(Sauti ya Thalja)

“Tunahitaji kila kitu, tunahitaji chakula, watoto wanahitaji chakula, Tuko watu 15 na wajukuu zangu ni yatima.”

WFP kufikia sasa imetoa mgao wa chakula kwa zaidi ya watu 83,000 wanaokimbia miji ya kaskazini mashariki mwa Syria. 

Aidha WFP inasaidia watu wanoishi kwenye makazi na mlo tayari huku jamii zinazowahifadhi zikipokea mgao wa chakula wa mara kwa mara, pia inafanya kazi na wadau kutathmini mahitaji ya watu katika makazi mapya yanayofunguliwa.

Margot Van Der Velden ni mkurugenzi wa masuala ya dharura kwenye WFP.

(Sauti ya Margot)

“Kile ambacho tumeshuhudia katika kipindi cha siku chache zilizopita ni mienendo ya watu kufuatia machafuko. Takriban watu 160,000 wamefurushwa. WFP imeweza kufikia watu 83,000 kati ya hao. Wengi wanaishi na jamii zinazowahifadhi, wengine katika makazi na tunafanya kila tuwezalo kufikia kundi lililosalia la watu ambao wamefurushwa kufuatia mzozo.”

Umoja wa Mataifa na wadau wanajiandaa kusaidia takriban watu 400, 000 ambao huenda wakahitaji msaada na ulinzi kutokana na mzozo.

 

TAGS: Syria, WFP, msaada wa chakula, Raqqa