Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watoto milioni 200, hawapati lishe toshelezi au ana uzito kupita kiasi- UNICEF Ripoti

Watoto wakikunywa uji wa mchele katika kituo kinachoendeshwa kwa msaada wa EU kweny jimbo la Phongsaly, Lao, PDR.
© UNICEF/Jacqueline Labrador
Watoto wakikunywa uji wa mchele katika kituo kinachoendeshwa kwa msaada wa EU kweny jimbo la Phongsaly, Lao, PDR.

Zaidi ya watoto milioni 200, hawapati lishe toshelezi au ana uzito kupita kiasi- UNICEF Ripoti

Afya

Idadi kubwa ya watoto wanateseka kutokana na lishe duni na mifumo ya chakula ambayo inawadumaza, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF katika ripoti kuhusu hali ya watoto duniani kwa mwaka huu wa 2019 ikiangazia zaidi watoto, chakula na lishe. 

Ripoti hiyo imetanabaisha kwamba takribani mtoto mmoja kati ya watoto watatu wenye umri wa chini ya miaka mitano au zaidi ya watoto milioni 200, hapati lishe toshelezi au ana uzito kupita kiasi. 

Halikadhalika watoto wawili kati ya watatu wenye umri wa kati ya miezi sita hadi miaka miwili hawapati chakula kinachosaidia makuzi ya haraka ya miili yao na ubongo na hivyo kuhatarisha makuzi duni ya ubongo, kushindwa kujifunza , kinga ya chini na ongezeko la maambukizi na mara nyingi vifo.

Akizungumzia ripoti hiyo MKurugenzi Mkuu wa UNICEF, Henrietta Fore amesema, "licha ya maendeleo ya kiteknolojia, kitamaduni na kijamii katika miongo chache iliyopita bado tumepoteza msingi muhimu. Iwapo watoto wanakula lishe duni, wanaishi maisha duni.”

"Anahoji iweje katika karne ya 21, iweje mtoto mmoja kati ya watatu amedumaa, ni wembamba kupindukia au tipwatipwa."

Bi. Fore ameongeza, “mamilioni ya watoto wanaishi kwa lishe duni kwa sababu hawana chaguo mbadala. Namna tunavyotazama na kukabiliana na mahitaji ya utapiamlo inapaswa kubadilika. Sio tu suala la kuwapa watoto chakula toshelezi,kubwa ni kuwapa chakula sahihi, hiyo ndio changamoto yetu ya pamoja leo.”

Ripoti imesema kwamba watoto milioni 149 wamedumaa, watoto milioni 50 ni wembamba sana kulingana na uzito wao, watoto milioni 340 wanakosa virutubisho muhimu ikiwemo vitamini na madini ya chuma.

Aidha kwa mujibu wa ripoti, watoto wengi katika miezi sita ya mwanzo hawapati maziwa ya mama pekee licha ya kwamba maziwa hayo yanaweza kuokoa maisha ya mtoto. 

Pia baada ya miezi sita ya mwanzo hadi miaka miwili takriban asilimia 45 hawali mbogamboga au matunda na zaidi ya asilimia 60 hawalishi mayai, bidhaa zitokanazo na maziwa, samaki au nyama.

Kadri mtoto anavyokuwa ndivyo anakutana na lishe duni

UNCEF imesema wakati watoto wanaendelea kukua wanapata lishe duni katika viwango vya juu kufuatia matangazo na uwepo wa vyakula vinavyotengenezwa katika muda mfupi.

Kwa mfano ripoti inasema asilimia 42 ya barubaru wanaohudhuria shule katika nchi za kipato cha chini na cha wastani wanakunywa karibu soda moja kwa siku na asilimia 46 wanakula chakula kinachotengenezwa kwa muda mfupi anagalau siku moja kwa wiki huku viwango hivyo vikiongezeka hadi asilimia 62 na 49 mtawaliwakwa barubaru katika nchi za kipato cha juu. Kwa mantiki hiyo idadi ya watoto walio na uzito kupita kiasi na utipwatipwa utotoni na barubaru inaongezeka kote duniani.

Kwa mujibu wa ripoti mzigo mkubwa wa lishe duni katika aina zake duni unabebwa na watoto na barubaru kutoka kwenye jamii masikini na zilizotengwa huku ikielezwa kuwa ni mtoto mmoja kati ya watano aliy kati ya miezi sita hadi miaka miwili kutoka nchi masikini anakula lishe yenye virutubisho tofauti kwa ajili ya makuzi bora.

Visababishi

Ripoti imesema kwamba majanga yatokanayo ma mabadiliko ya tabianchi yanasababisha ukosefu wa chakula, ukame kwa mfano unasababisha asilimia 80 ya madhara na uharibifu katika kilimo na kuathiri chakula kilichopo kwa ajili ya watoto na familia, vile vile kiwango na bei ya chakula.

Muarobaini wa hali ya sasa

Ili kukabiliana na janga hilo, Bi Fore amesema vita hivi sio vya mtu mmoja na ushiriki wa serikali ni muhimu, sekta binafsi na mashirika ya kiraia kukabiliana na mienendo ya lishe duni katika sura zake tofauti.

UNICEF imetoa wito kwa wadau kuwezesha familia, watoto na vijana kuchagiza kupat lishe nora ikiwemo kwa kuimarisha elimu kuhusu lishe na kuweka sheria kwa mfano kodi ya bidhaa za uskari na kupunugza mahitaji ya vyakula vyenye lishe duni na kuhakikisha vyakula vyenye bei nafuu na kujenga mazignira ya lishe bora kwa watoto na barubaru.