Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano kaskazini-mashariki mwa Syria, watoto 11 wauawa, 70,000 wakimbia makazi yao- Unicef

Picha hii ya tarehe 11 Oktoba 2019 ikimuonyesha mwanamke mmoja raia wa Syria akiwa na mwanae na familia yake baada ya kukimbia mji wa Ras al-Ain na kuwasili hapa eneo la Tal Tamer kufuatia mashambulizi kaskazini-mashariki mwa Syria.
© UNICEF/Delil Souleiman
Picha hii ya tarehe 11 Oktoba 2019 ikimuonyesha mwanamke mmoja raia wa Syria akiwa na mwanae na familia yake baada ya kukimbia mji wa Ras al-Ain na kuwasili hapa eneo la Tal Tamer kufuatia mashambulizi kaskazini-mashariki mwa Syria.

Mapigano kaskazini-mashariki mwa Syria, watoto 11 wauawa, 70,000 wakimbia makazi yao- Unicef

Msaada wa Kibinadamu

Tangu kuanza kwa mashambulizi mapya kaskazini-mashariki mwa Syria tarehe 9 mwezi huu wa Oktoba, takribani watoto 70,000 wamekimbia makazi yao, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto,  UNICEF.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema kwa sasa idadi kubwa ya watoto hao wamesaka hifadhi kwa ndugu, jamaa na marafiki na kwamba vituo 30 vya makazi ya dharura, zikiwemo shule na mapagala zimebainishwa kama maeneo ya hifadhi katika miji ya Hasakeh, Raqqa na Tal Tamer.

“Kwa sasa vituo hivyo ni hifadhi ya watu 3,400, ingawa idadi inabadilika kwa kuwa watu hawakai muda mrefu wanaondoka,” amesema Marixie Mercado, msemaji wa UNICEF Geneva, Uswisi akiongeza kuwa shirika hilo linafanya kila iwezalo kutoa misaada ya dharura kwa familia zinazowasili kwenye vituo hivyo.

Madhara kwa watoto na kiwango cha uharibifu wa miundombinu ya kijamii

Hadi sasa watoto wapatao 4 wameuawa na 9 wamejeruhiwa kaskazini-mashariki mwa Syria ilihali watoto 7 wameripotiwa kuuawa huko Uturuki.

“Watoto wapatao 170,000 wanaweza kuhitaji msaada wa kibinadamu kutokana na mapigano na kwamba kituo cha kusambaza maji kwa watu 400,000 kilicho  Alouk huko Hasakeh bado hakitoi huduma,” amesema Bi. Mercado akiongeza kuwa, “mafundi waliweza kutathmini kiwango cha uharibifu na kufanya matengenezo jana, bado kituo hicho hakiwezi kutoa huduma ya maji kutokana na nyaya za umeme haziwezi kutengenezwa.”

UNICEF inaongeza kuwa kituo mbadala cha kusambaza maji kinaweza kukidhi mahitaji kwa asilimia 30 pekee huko Hasakeh na kwamba visima vilivyopo vya maji si virefu kutosha kuweza kuwa na maji safi na salama, “kwa hiyo ni muhimu kituo cha kusukuma maji cha Al  Houk kikatengamaa haraka ili kiweze kurejea kutoa huduma.”

Msemaji huyo amesema UNICEF kwa  upande wake itakuwa inasambaza mafuta kwa ajili ya jenereta zinazoweza kutumiwa iwapo umeme utakatika, halikadhalika kusafirisha maji kwa lori kwenda kwenye vituo vya makazi ya wakimbizi wa ndani.

Mtoto katika kituo cha utambuzi kwenye kijiji cha Sahel nchini Iraq ambako wasyria 182 wamevuka mpaka na kuingia kufuatia mapigano mapya kaskazini-mashariki mwa nchi yao. Wakimbizi hawa wanapata msaada kutoka IOM. (Oktoba 2019)
IOM/Vanessa Okoth-Obbo
Mtoto katika kituo cha utambuzi kwenye kijiji cha Sahel nchini Iraq ambako wasyria 182 wamevuka mpaka na kuingia kufuatia mapigano mapya kaskazini-mashariki mwa nchi yao. Wakimbizi hawa wanapata msaada kutoka IOM. (Oktoba 2019)

Shule nazo hazijaepukika kwenye janga hili

Bi. Mercado amesema shule moja huko Tal Abiad imeshambuliwa na kwamba huko Ras Al-Ain, shule, kliniki na masoko yamefungwa tangu tarehe 9  mwezi huu wa Oktoba.

Ameongeza kuwa tarehe 13 mwezi huu wa Oktoba, mashambulizi yaliripotiwa kwenye kambi ya Ein Issa, kambi ambayo ni makazi ya watu 13,000 wakiwemo watoto 8,000. “Idadi ya watu isiyojulikana wanaweza kuwa walikimbia kutoka kambini hapo. Watoto 27 wenye  umri wa kati ya miaka 2 hadi 14 na wasioambatana na wazazi, wakiwemo 24 ambao ni wageni wamehamishiwa mji wa Al Raqqa ambapo hii leo timu ya UNICEF inawatembelea kufahamu hali zao.”

Ghasia zikishamiri, hamisheni raia wenu wakiwemo watoto

Kadri ghasia zinavyozidi kushamiri, UNICEF imerejelea wito wake kwa pande kinzani kwenye mzozo huo na wale wenye ushawishi walinde watoto kila wakati.

“Wale wanaopigana kaskazini-mashariki mwa Syria na kwingineko nchini humo, lazima walinde raia na miundombinu ya kijamii na wasiitumie miundombinu hiyo kujinufaisha kijeshi,” amesema Bi. Mercado.

Halikadhalika amesema kadri hali ya usalama inavyozidi kudorora, UNICEF inatoa wito kwa nchi wanachama kuhamisha haraka iwezekanavyo raia wao, wakiwemo watoto ili waweze kulindwa dhidi ya madhila.