Theluthi moja ya chakula cha binadamu duniani hupotea kila mwaka- FAO

Mradi wa FAO wa uhakika wa chakula (PESA) katika sekta ya kilimo, mifugo, maendeleo vijijini, uvuvi na kilimo
© FAO-Magnum Photos/Alex Webb
Mradi wa FAO wa uhakika wa chakula (PESA) katika sekta ya kilimo, mifugo, maendeleo vijijini, uvuvi na kilimo

Theluthi moja ya chakula cha binadamu duniani hupotea kila mwaka- FAO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katika kuelekea siku ya chakula duniani ambayo kila mwaka hufanyika Oktoba 16, shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO, limesema kila mwaka theluthi moja ya chakula kinachozalishwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu kina pote bure au kutupwa. Maelezo zaidi na Flora Nducha

Kwa mujibu wa ripoti ya FAO iliyotolewa leo kuhusu mada hiyo inasema upotevu wa chakula na kutupwa kwa chakula kuna madhara makubwa kwa uchumi , uhakika wa chakula na mazingira. Ripoto hiyo mpya  iliyopewa jina SOFA 2019  katika mnyororo wa thamani wa chakula, inafafanua kwa kina wapi chakula hicho kinapotea au kutupwa zaidi kuanzia shambani kwa mkulima hadi mezani kwa mlaji na nchi zinachukua hatua gani kukabiliana na upotevu wa chakula au utupwaji wa chakula. Adrea Cattaneo ni afisa wa masuala ya kiuchumi ya FAO anaanza kwa kufafanua tofauti ya upotevu wa chakula na utupwaji wa chakula

(SAUTI YA CATTANEO)

“Upotevu wa chakula kwa mujibu wa FAO hutokea kuanzia baada ya mavuno bila kujumisha mauzo, na upotevu huu unaweza kufanyika na wakulima, mchakato wa uandaaji na wale wanaofanya katika sekta ya usafirishaji kwa ajili ya uuzaji wa chakula , na utupwaji wa chakula kwa upande mwingine hutokea katika ngazi ya soko baina ya muuzaji na mtumiaji. Na tofauti baina ya upotevu na utupwaji wa chakula ni muhimu kwa sababu watu wana malengo tofauti.

Amesema mahali kunakoongoza kwa upotevu mkubwa wa chakula ni Kusini na katikati mwa Asia ambako ni asilimia 21 , lakini pia Amerika Kaskazini na Ulaya ambako ni asilimia 16. Na sasa nini kifanyike kuzuia hali hii  Cattaneo amesema

(SAUTI YA CATTANEO)

“Kitu cha kwanza kabisa watu wanatakiwa kufahamu kuhusu upotevu na utupwaji wa chakula kitu kitakachoisaidia kuchukua hatua , kwetu kama watu binafsi na pia watunga será, kuwekeza katika miundombinu inayohitajika, kuitaarifu jamii kuhusu hatua za kupunguza upotevu na utupwaji wa chakula na katika baadhi ya nchi kufanyia mabadiliko ruzuku ya chakula ambazo bila kukusudia zinaweza kuchangia upotevu na utupaji zaidi wa chakula.”

Wakati chakula hicho kikiendelea kupoteza ama kutupwa FAO inasema kuna watu milioni 820 kote duniani wanaokabiliwa na njaa.