Kuna hatua katika kudhibiti majanga kasi zaidi inahitajika:Guterres

13 Oktoba 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuna hatua zinazopigwa kote duniani katika kudhibiti hatari ya majanga lakini ametoa wito kwa kuongeza jitihada zaidi hususani kuwasaidia jamii zisizojiweza.

Katika ujumbe wake maalum wa siku ya kimataifa ya kupunguza hatari ya majanga ambayo huadhimishwa kila mwaka Oktoba 13 Guterres amesema “katika maisha yangu yote na kazi zangu mimezuru jamii nyingi zilizoathiriwa na matukio mabaya ya hali ya hewa na majanga mengine ya asili. Kuanzia Pasifiki Kusini hadi Msumbiji, mpaka Caribbea na zaidi, nimejionea uharibifu na athari zilizobadili maisha kutokana na dharura ya mabadiliko ya tabianchi kwa jamii zisizojiweza.”

Ameongeza kuwa majanga yanasababisha madhara makubwa na yanaweza kwa muda mfupi kufuta miongo ya maendeleo yaliyopatikana. Katika muongo ujao amesema dunia itawekeza matrilioni ya dola katika makazi mapya, shule, hospitali na miundombinu. Na kwamba “mnepo dhidi ya tabianchi na upunguzaji wa hatari ya majanga ni lazima viwe kiini cha uwekezaji huu.”

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa kuna suala la msingi la kiuchumi kwa hatua kama hizo: kufanya miundombinu kuwa na mnepo zaidi dhidi ya tabianchi kunaweza kuwa na faida za uwiano wa sita kwa moja kwa kila dola inayowekezwa , dola sita zinaweza kuokolewa.

“Hii inamaanisha kwamba uwekezaji katika mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi unaunda ajira na kuokoa fedha. Na ni kitu sahihi kufanya:kinaweza kupunguza na kuzuia madhila kwa binadamu.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres akitembelea darasa za shule ya June 25 mji wa Beira nchini Msumbiji, shule ambayo iliharibwa na kimbunga Idai.
UN Mozambique
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres akitembelea darasa za shule ya June 25 mji wa Beira nchini Msumbiji, shule ambayo iliharibwa na kimbunga Idai.

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema anatiwa moyo na uungwaji mkono wa kimataifa kwa ajili ya hatua dhidi ya tabianchi na kwa ahadi nyingi zilizotolewa hivi kaiibuni kwenye mkutano wa hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

“Sote ni lazima sasa tuangalie kuongeza matamanio. Natoa wito kwa ulimwengu kuongeza uwekezaji wao ifikapo 2020 na kuhakikisha kwamba kupunguza hatari za majanga kunapewa kipaumbele katika Muungo wa kuchukua hatua. Hebu sote tuazimie kwa hamu kubwa juu ya hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, kupunguza hatari za majanga na kuelekeza juhudi zetu zote katika kufikia Malengo ya maendeleo endelevu.”

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter