Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 25 baada ya azimio la Beijing mafanikio yapo lakini watoto wengi wa kike hawazijui haki zao

Mwanafunzi wa kike nchini Uganda akiwasiliana na wanafunzi wenzake
© UNICEF/Zahara Abdul
Mwanafunzi wa kike nchini Uganda akiwasiliana na wanafunzi wenzake

Miaka 25 baada ya azimio la Beijing mafanikio yapo lakini watoto wengi wa kike hawazijui haki zao

Haki za binadamu

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya mtoto wa kike duniani ambapo mwaka huu dunia inasherehekea hatua ambazo zimefikiwa tangu kupitishwa kwa azimio la Beijing lililotambua haki za mwanamke na mtoto wa kike kuwa ni haki za binadamu takribani miaka 25 iliyopita. Kila nchi imechukua hatua mbalimbali kutekeleza azimio hilo ikiwemo Tanzania.

Mbwana Salum Katondo, kiongozi wa taasisi ya Masasi youth development network  ya nchini humo akihojiwa na Deo Mpokasye wa redio washirika Fadhila ya Masasi Mtwara, anasema hatua zimepigwa katika kupambania haki za mtoto wa kike Wilaya ya Masasi mkoani humo lakini bado watoto wenyewe wa kike hawazijui haki zao,“ni asilimia chache sana ya watoto wa kike wanaotambua haki zao. Kuna hiyo changamoto ya watoto wa kike kutojua haki zao hasa wale waliko shuleni na hata walioko nje ya shule. Kwa upande wetu kazi yetu kubwa ni kuelimisha vijana wazitambue haki zao za msingi ili waweze kufanya shughuli zao kwa kutambua haki na wajibu wao.”

Naye Farida Musa wa taasisi ya Talia inayohusika na elimu kwa vijana hasa watoto wa kike akieleza hatua zilizopigwa hususani upande wa mimba za utotoni kusini mwa Tanzania anasema,“mimba za utotoni kwa huku kusini hapo zamani zilikuwepo, na zipo bado lakini zinapungua. Hiyo yote ni kulingana na elimu tunayoitoa kama kwenye vijiwe, shuleni na mikutano ya hadhara.”