Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR nayo yampongeza Waziri Mkuu Ahmed

Wakimbizi kutoka jimbo la Blue Nile wakilikimbia eneo hilo kuingia Ethiopia. Ethiopia ni moja ya nchi za Afrika zinazohifadhi wakimbizi wengi
UN
Wakimbizi kutoka jimbo la Blue Nile wakilikimbia eneo hilo kuingia Ethiopia. Ethiopia ni moja ya nchi za Afrika zinazohifadhi wakimbizi wengi

UNHCR nayo yampongeza Waziri Mkuu Ahmed

Amani na Usalama

Wakati huo huo, Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi naye amepaza sauti kufuatia Waziri Mkuu Ahmed kushinda tuzo ya amani ya Nobel.

Bwana Grandi akinukuliwa kupitia taarifa iliyotolewa na UNHCR mjini Geneva, Uswisi amesema, “hatua ya leo ya kumtuza Waziri Mkuu Ahmed tuzo ya amani ya Nobel ni ushahidi mkubwa wa juhudi zake za kuleta amani kwenye ukanda wake na duniani kwa ujumla.”

 Kamishna huyo mkuu wa UNHCR amesema Ethiopia kwa muda mrefu imekuwa na historia ya kukaribisha na kuhifadhi wakimbizi kutoka maeneo mbali mbali ya ukanda huo na kwamba, “kwa kuruhusu wakimbizi kutangamana vyema kwenye jamii, nchi hiyo siyo tu inatekeleza wajibu wake wa kimataifa wa kibinadamu bali pia ni mfano wa mataifa mengine  yanayokaribisha wakiambizi duniani.”

Bwana Grandi amesema wao UNHCR wanajivunia kumhesabu kama miongoni mwa waandaaji wa jukwaa lijalo la kimataifa la wakimbizi litakalofanyika mwezi Disemba mwaka huu na wanampongeza kwa dhati Waziri Mkuu Ahmed, wananchi wa Ethiopia na kamati ya Nobel.