Kinachoendelea Burkina Faso kinaathiri ukanda mzima wa Sahel

11 Oktoba 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linaungana na wadau wake kuonya juu ya janga linalochipukia huko maeneo ya kaskazini na kati mwa Burkina Faso.

Msemaji wa UNHCR mjini Geneva, Uswisi, Andrew Mbogori amewaambia waandishi wa habari hii leo ya kwamba, “kila uchao maisha ya mamia ya maelfu ya watu yanakumbwa na mshikemshike kutokana na ghasia na ukosefu wa usalama.”

 Bwana Mbogori amesema takribani watu 486,000 wamelazimika kukimbilia maeneo mengine ya nchi hiyo, ambapo kati yao hao, 267,000 wamefurushwa katika kipindi cha miezi 3 iliyopita.

“Wengine 16,000 ni wakimbizi nchi jirani. Ghasia za kijeshi zinazoendelea zinasababisha dharura ya kibinadamu huko ukanda wa Sahel,” amesema Bwana Mbogori.

Amezungumzia kile walichoshuhudia walipotembelea eneo la Kaya, kaskazini-mashariki mwa mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou, na Barsalogho, kwenye jimbo la kati la Sanmatenga ambako amesema, “tulishuhudia madhara ya matukio ya kutisha ya hivi karibuni kwa waathirika. Maelfu ya watu wanakimbia na wanajaribu kusaka usalama kwa wenyeji au kwenye vituo vya mpito.”

Amesema matumaini ya watu hao kurejea nyumbani ni finyu na matokeo y ake mahitaji yao na yale ya familia zinazowahifadhi kama vile chakula, yanaongezeka.

Visa vya kikatili vilivyokumba watu hao ni pamoja na wenzao zaidi ya 500 kuuawa katika mashambulizi 472 mwaka jana huku miundombinu ya kijamii ikiwa imesambaratishwa.

UNHCR inasema kwamba kwa kuwa Burkina Faso  yenyewe inahifadhi wakimbizi wanaokimbia ghasia nchini mwao ikiwemo Mali, mahitaji ya kibinadamu yanaongezeka wakati huu ambapo, “vikundi vilivyojihami vimeimarisha mashambulizi yao huko Burkina Faso na nchi jirani za Mali na Niger. Maeneo yanayozunguka nchi hizi tatu ni maeneo mapya ya ghasia.”

Shirika hilo limesema mashambulizi tayari yameingia hadi Benin.

Kwa ujumla UNHCR inasema zaidi ya watu milioni 5.4 kwenye ukanda huo wanahitaji misaada ya dharura wakiwemo milioni 3.2 nchini Mali, na  700,000 huko Niger magharibi.

Bwana Mbogori amesema kandoni mwa mkutano wa mwaka wa kamati tendaji ya UNHCR uliofanyika wiki hii, Kamishna Mkuu wa shirika hilo alishuhudia jinsi wawakilishi kutoka Burkina Faso, Mali, Niger, Chad na  Mauritania walivyosisitiza azma ao ya kushirikiana ili kushughulikia janga la ukimbizi na kuhakikisha watu waliokimbia wanweza kurejea nyumbani salama.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter