Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waziri Mkuu wa Ethiopia ashinda tuzo ya amani ya Nobel, Guterres azungumza

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed akihutubia siku ya uhuru wa habari mwaka 2019 mjini Adis Ababa Ethiopia
UNESCO/Vintage Pixels
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed akihutubia siku ya uhuru wa habari mwaka 2019 mjini Adis Ababa Ethiopia

Waziri Mkuu wa Ethiopia ashinda tuzo ya amani ya Nobel, Guterres azungumza

Amani na Usalama

Tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka 2019 ametuza Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kwa juhudi zake za kuimarisha amani na ushirikiano wa kimataifa.

Kufuatia tangazo hilo hii leo na kamati ya tuzo za Nobel, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amempongeza huku akisema kuwa “mara nyingi nimekuwa nasema kuwa upepo wa matumaini unavuma kwa kasi kubwa barani Afrika. Waziri mkuu Ahmed ni moja ya sababu za kuwepo kwa upepo  huo.”

Kupitia taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake jijini New York, MArekani, Bwana Guterres ambaye yuko ziarani Denmark amesema kwamba dira ya Waziri Mkuu huyo imesaidia maridhiano ya kihistoria kati ya Ethiopia na Eritrea na “ilikuwa ni heshima kubwa kwangu kushuhudia utiaji saini wa makubaliano ya amani mwaka jana.”

Guterres amesema hatua hiyo ya kihistoria imefungua fursa mpya kwenye ukanda huo wa pembe ya Afrika ya kuweza kufurahia usalama na utulivu na kwamba, “uongozi wa Waziri Mkuu Ahmed umeonesha mfano bora kwa wengine Afrika na kwingineko wa kuachana na yaliyopita na kuweka mbele maslahi ya watu.”

Mkataba huo wa amani kati ya Ethiopia na Eritrea ulimaliza mzozo wa miaka 20 kati yao kufuatia vita vya mpakani vya m waka 1998 hadi 2000.

Waziri Mkuu huyo wa Ethiopia anakuwa mshindi wa 100 wa tuzo hiyo ya amani ya Nobel na atatunukiwa mwezi Disemba mwaka huu.

Mshindi wa tuzo hupatiwa pia fedha taslim dola takribani 900,000.