Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa si muafaka kupeleka kikosi cha kulinda amani Syria- Guterres

Wakimbizi wa Syria wakiwa mbioni kutafuta makazi
UNICEF/UN0277723/Souleiman
Wakimbizi wa Syria wakiwa mbioni kutafuta makazi

Sasa si muafaka kupeleka kikosi cha kulinda amani Syria- Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza huko mjini Copenhagen Denmark hii leo amekumbusha kuwa operesheni zozote zile za kijeshi ni lazima zizingatie katiba ya Umoja wa Mataifa, na sheria za kibinadamu za kimataifa.

Guterres amesema hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliohudhuriwa pia na Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen punde baada ya kushiriki mkutano wa dunia wa mameya.

Kauli hiyo inafuatia mashambulizi ya kijeshi ya jana Oktoba 9 huko kaskazini-mashariki mwa Syria, akisema “yanazidi kufanya mzozo wa Syria kuwa mbaya zaidi.”

Guterres amesema haamini kwenye suluhu la kijeshi kwenye mzozo Syria na kwenye mzozo wowote ule duniani na kwamba suluhu anayoamini  yeye ni ile ya njia  ya kisiasa.

Amegusia mwelekeo wa suluhu ya kisiasa kupitia azimio namba 2254 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo hata leo limekutana kwa dharura kuhusu Syria.

Hata hivyo amesema, “jambo moja lililo dhahiri ni kwamba suluhu yoyote ya mzozo wa Syria itahitaji kuheshimu mamlaka, mipaka na umoja wa Syria.”

Alipoulizwa na wanahabari pendekezo la kupeleka kikosi cha ulinzi wa amani iwe ni kutoka Ulaya au walinda amani wa Umoja wa Mataifa Katibu Mkuu amesema, “tatizo la kikosi cha ulinzi wa amani kama jina lenye linavyosema, unahitaji kuwa na amani ili kuitunza. Huwezi kuwa na kikosi cha ulinzi wa amani ambako hakuna amani ya kutunza.”

Katibu Mkuu amesema kikosi cha ulinzi wa amani mara zote ni matokeo ya makubaliano ya kisiasa, na kuwepo na amani ya kutunza na hivyo kikosi hicho kinakuwa na dhima muhimu.

“Bado  hatujafikia hapo, naamini hivyo, kwa sasa tunachopaswa kufanya ni kuhakikisha kuwa mapigano yanakoma nchini Syria. Na bila shaka nina wasiwasi kinachoendelea mashariki mwa Syria na bila shaka Idlib,” amesema Katibu Mkuu.