10 Oktoba 2019

Huduma za posta duniani zikitimiza miaka 145, tumesaka maoni ya watu juu ya huduma hizo wakati huu ambapo baadhi wanasema tayari imejichimbia kaburi ilihali wengine wanasema ndio kwanza inashamiri.

Juvenary Kajara mkazi wa Dar es Salaam Tanzania anaanza kwa kueleza kuwa hapo zamani  watu wengi walipashana habari kwa njia ya posta. Yaani mawasiliano muhimu zaidi yalifanyika kwa njia hiyo.

Kajara anaeleza kuwa zilikuwepo njia mbalimbali za utumaji wa vifurushi na mizigo miepesi,

Ninakumbuka njia kuu mbili au tatu zilizo kuwa zinatumika. Kulikuwa na njia ya Telegram, Register na njia ya kawaida. Hii ilikuwa miaka ya 1980 hivi. Telegram na Register zinatumika hadi sasa na faida zake ilikuwa ni uhakika wakufika kwa mzigo - Juvenary Kajara

Aidha  bwana Kajara, anaendelea kueleza kuhusu faida za mfumo huu wa Telegram na Register ambapo anasema ni pamoja na kukuza uchumi kwa taifa kwani kwa kila mzigo unaotumwa mtumaji hana budi kununua stamp sawa sawa na thamani ya pesa ya kusafirisha mzigo huo, hiyo serikali inapata kodi kupitia ununuzi wa stamp.

Hata hivyo ana mashaka kiasi na namna njia ya kawaida ya utumaji  barua au fedha ulivyokuwa wa mashaka wakati huo na anatoa mfano,

“njia ya kawaida ilikuwa ni nzuri lakini changamoto zake ni pamoja na kutokuwepo uhakika wa kupata mzigo kwa wakati. Ninakumbuka mwaka 1992 nilitumiwa pesa kupitia majarida, takribani dola 50 za kimarekani.  Sikuzipata, ingawa nilipata jarida tu na lilikuwa tayari limefunguliwa. Hivyo baadhi ya taarifa  muhimu wakati fulani zilikuwa zinapotea kupitia mfumo wa kawaida wa utumaji wa barua.”

Lakini Bwana Kajara anaeleza kuwa suluhisho la wakati huo lilikuwa ni kulipia sanduku lako binafsi la barua ambapo barua zingekufikia moja kwa moja ingawa visanduku hivyo vilikuwa mbali na makazi ya watu na hivyo ungelazimika kufunga safari za mara kwa mara ili kwenda kuchungulia kama kuna chochote kilichotumwa.

“Kwa ufupi kulingana na ushindani ulivyo, mashirika ya posta na simu yamepata changamoto kupitia mitandao mingi imara na madhubuti ya mawasiliano, hivyo kwa sasa posta zinatumika kutuma barua za kuomba ajira na tenda japo si mara nyingi sana.” Anahitimisha Bwana Kajara.

Naye Mzee Cyril Pesha, mwanasheria na mkazi wa Dar es Salaam Tanzania akichangia katika mjadala huu unaoangazia historia ya mawasiliano na huduma za Posta, anathibitisha maelezo ya Bwana Kajara kwa kusema,

“maelezo ya Kajara ni sahihi. Telegramu ilirithiwa na Teleksi na baada ya Teleks ulifuata mfumo wa facsímile au fax na sasa hivi kuna intaneti na  ‘scanned message’.”

Posta ya Umoja wa Mataifa (UNPA)
Stempu iliotolewa na mamlaka ya posta ya Umoja wa Mataifa Julai 18, siku ya Mandela: Mchoraji Martin Mörck (Norway). muundaji: Rorie Katz (Umoja wa Mataifa)

Judith Blasio mkazi wa Karagwe Kagera Tanzania anaeleza uzoefu wake wa nchi za Ulaya akisema, “nchi zilizoendelea, matumizi ya posta kwa wananchi ni muhimu kwani simu za ndani, intaneti, taarifa za serikali mathalani, malipo ya maji, umeme au hata magazeti unaletewa hadi nyumbani. Hata magazeti yanayotangaza biashara. Hii ni kwasababu usajili watu na makazi vimepangwa vizuri.”

Mchangiaji mwingine akieleza namna fedha zilivyokuwa zikitumwa kwa njia ya posta kabla ya mifumo ya sasa kuanzishwa anasema,

Fedha zilikuwa zinatumwa kwa njia ya TMO yaani Telegraphic Money Orders. Ambapo mathalani ikiwa mzazi anataka kumtumia mtoto wake aliyeko shule ni mbali, basi anapeleka fedha posta iliyokaribu naye, hiyo posta inapiga simu kwenye posta iliyo karibu na mpokeaji, wanampatia kiasi cha fedha kilichokabidhiwa upande wa pili.- Mkazi wa Karagwe

Mwalimu Melchior Nkobelerwa anakubaliana na maelezo ya wengine na anasema umuhimu wa posta bado upo lakini anashauri kubadili mfumo ili kuteka hisia na matakwa ya wateja akisema,

"zamani posta iliwika kwa kuwa ilikuwa posta na simu (Tanzania). Kutenganishwa tu ndipo mambo yalienda mrama. Simu zikateka nafasi. Telegram ikatekwa na meseji, telefax ikatekwa na barua pepe na kadhalika. Umuhimu wa barua bado upo, unaandika ujumbe mrefu na kuandika P.T.O na inatunzwa kwa marejeleo ya baadaye. Posta sasa hapa ina sajili magazeti, ina ushirika the Western Union na ina benki yaani postal bank. Stamps zilitangaza vivutio vya nchi kama wanyama, wanamichezo (Bayi,Nyambui, Nzael Kyomo)na wengine."

Wachangiaji wengine wa mjadala huu wanaeleza kuwa suala jingine lililo ziangusha huduma za posta ilikuwa ni kuchelewa kwa mizigo, mchangiaji mmoja anatoa mfano unaoungwa mkono na wengi kuwa mara kadhaa akiwa mbali aliandika barua kuzituma nyumbani, lakini angeweza kusafiri miezi baadaye na kufika nyumbani kabla barua alizoandika hazijafika.

Mwalimu Straton Ruhinda, mkufunzi katika vyuo vikuu nchini Tanzania anayebobea katika masuala ya sosholojia na antropolojia anaelezea historia fupi ya huduma za posta hasa mkoa wa Kagera kwamba zilianza tangu ukoloni wa mjerumani. Hata jengo dogo la posta ya kwanza enzi za mjerumani mkoani Kagera, huko Tanzania, bado lipo. Anasema,

“Kwa hakika posta lilikuwa(na bado ni)  muhimu kwa katika maisha ya watu wa dunia nzima”

Mwalimu Ruhinda anaeleza kuwa posta ilikuwa kiungo muhimu kwa mawasiliano ya barua japo wakati mwingine zilikuwa zinachelewa ila kwa uaminifu zinafika. Sababu ya kuchukua muda mrefu kumfikia muhusika mpaka ikapewa jina snail mail. Pamoja na hayo, anaeleza kuwa posta iliwasaidia watu hata kupata elimu kwani walikuwa wanapokea masomo yao na hata kufanikiwa kuhitimu masomo yao.

“Posta walikuwa hawapotezi barua ya mtu labda iwe bahati mbaya sana.” Anakumbuka Mwalimu Ruhinda. “Nakumbuka Baba yangu mwaka 1986 alipokea barua kutoka Uganda iliyokuwa imeandikwa miaka miwili nyuma. Kilichotokea ni kuwa mzee alikuwa anaishi Dar es salaam hadi mwaka 1975 alipopata uhamisho kwenda Kondoa mkoani Dodoma, kisha mkoani Kigoma na baadaye mjini Bukoba. Miongoni mwa marafiki zake aliokuwa nao Dar es salaam alikuwepo mtu mmoja kutoka nchini Uganda. Mtu huyo, mnamo mwaka 1983 akiwa Uganda alimuandikia mzee barua kwa anwani ya Dar es Salaam ambako tayari mzee alikuwa ameshahama miaka 10 nyuma na hata shirika alililokuwa akifanyia kazi lilishavunjwa. Barua ilipofika Dar es Salaam, kwenye  sanduku la barua lililolilokuwa likimilikiwa na shirika lililokuwa mwajiri wa mzee wangu ilionekana huyo mtu alihamia kondoa, hivyo wakairejesha posta na kuandika “Try Kondoa” yaani jaribu Kondoa, ambapo hali kadharika ilipopokelewa waliandika, jaribu Kigoma baada ya kujua kuwa mtu huyo alielekea Kigoma, na baadaye Bukoba. Barua ilipofika Bukoba kwa mwendo huo huo wa 'Jaribu kule,' hatimaye ilimfikia akiwa Karagwe, miaka miwili tangu ilipoandikwa"

Ruhinda anatoa ushauri kwa posta kuwa ili katika zama za hivi sasa iweze kuendelea inabidi kubadili mfumo wake wa sasa kwani vado changamoto zipo, akitoa mfano, “mwezi Januari mwaka  huu 2019 nilihitaji kitabu fulani kinapatikana Marekani. Jamaa yangu akakinunua kule Marekani na akakiweka posta. Baada ya muda tukahisi kimepotea maana miezi ilipita na kitabu hakifiki. Ndugu yangu Yule akanunua kitabu kingine na kupatia mtu aliyekuwa anasafiri kuja Tanzania na akanipatia kwa mkono. Mwezi wa tisa ndio kile kitabu kilichowekwa Posta kilifika, yaani miezi tisa kipo njiani!! Hakika ni Snail Mail!”

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud