Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Visa vya Ebola vimesalia katika eneo dogo lakini lenye changamoto nyingi-WHO

Mhudumu wa afya wa Ebola akionesha ishara kuwa watu wa DRC hawapaswi kuwaogopa madaktari isipokuwa ugonjwa wenyewe wa Ebola (aGOSTI 2019)
UN Photo/Martine Perret
Mhudumu wa afya wa Ebola akionesha ishara kuwa watu wa DRC hawapaswi kuwaogopa madaktari isipokuwa ugonjwa wenyewe wa Ebola (aGOSTI 2019)

Visa vya Ebola vimesalia katika eneo dogo lakini lenye changamoto nyingi-WHO

Afya

Visa vya maambukizi ya Ebola vimeendelea kupungua na kusalia katika eneo dogo ingawa hatuwezi kusema tumemaliza vita dhidi ya ugonjwa huu kwani bado tunakabiliana na changamoto kadhaa, Dkt Michael Ryan, Mkurugenzi Mkuu anayesimamia programu za dharura katika shirika la afya duniani WHO amewaeleza wana Habari mjini Geneva Uswisi hii leo.

Dkt Ryan akieleza alichokishuhudia alipokuwa ziarani nchini jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, amesema,

“tunafurahi kwa hatua zilizopigwa. Chini ya uongozi wa DRC na wadau tumemudu kuubana ugonjwa na kusalia katika eneo dogo la pembe tatu maeneo ya Mambasa, Komanda, Beni na Mandima ambako ni eneo kati ya Kivu kaskazini na Ituri.”

Hata hivyo Dkt Ryan ameeleza kuwa pamoja na kuwa taarifa za ugonjwa kusalia katika eneo dogo ni taarifa chanya, lakini pia ni kwamba ugonjwa huo umesogea katika maeneo yasiyo na usalama.

“Mafanikio yamekuwa kuusukuma ugonjwa nje ya Butembo, Katwa na Beni lakini sasa ugonjwa uko katika maeneo ya vijijini zaidi na yasiyo na usalama lakini angalau kiwango cha maambukizi ni kidogo.”

Aidha Mkurugenzi huyo wa masuala ya dharura ya WHO ameeleza kuwa Ebola imeonekana kurejea katika maeneo ilikoanzia.

“ukifikiria kuhusu Mandima ambako ndiko chanzo cha ugonjwa. Virusi viliambukiza katika eneo la Mandima kwa miezi minne au mitano kabla ya kutambulika katika hospitali ya Mangina. Kwa hivyo kimsingi, ugonjwa umerejea katika ukanda huo.”

Vile vile Dkt Ryan amesema changamoto kuwa waliyonayo ni kutekeleza majukumu yao katika maeneo yasiyo na usalama na hivyo akatoa wito kwa wadau wa usalama kama ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani DRC, MONUSCO na wengine kuendelea kuwasaidia katika suala la usalama ili kuzifikia jamii.

Dkt Ryan ameeleza kuwa ni visa 14 ambavyo vimeripotiwa Kivu Kaskazini na Ituri tangu tarehe 30 ya mwezi Septemba hadi kufikia wiki ya kwanza ya mwezi huu wa Oktoba yaani tarehe 6 Oktoba ikilinganishwa na visa 20 vya wiki ya tarehe 23 hadi 29 ya mwezi Septemba.

Kwa takwimu hizo, idadi ya visa vipya vilivyothibitika, imekuwa ikipungua tangu wiki ya tarehe 9 hadi 15 mwezi Septemba wakati visa 51 viliporipotiwa.

Viwango vya juu kabisa katika mwaka huu wa 2019 ilikuwa vilivyotokea katika wiki ya tarehe 22 hadi 28 mwezi Aprili wakati viliporipotiwa visa 126.