Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulio mapya nchini Syria yalaaniwa

Ru'a mwenye umri wa miezi 18, akiwa juu ya baiskeli ya babu yake wakati wakivuka eneo la Mesraba huko Ghouta Mashariki nchini Syria
UNICEF/2018/Amer Almohibany
Ru'a mwenye umri wa miezi 18, akiwa juu ya baiskeli ya babu yake wakati wakivuka eneo la Mesraba huko Ghouta Mashariki nchini Syria

Mashambulio mapya nchini Syria yalaaniwa

Amani na Usalama

Nchini Syria mashambulio mapya yaliyofanywa kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo yameibua kauli za kulaani, zikisema kuwa wasyria wamechoka na hawahitaji mashambulio zaidi wakati huu ambao bado wako kwenye majanga.

Tangu mwezi Machi mwaka 2011, wasyria wamekuwa wakihamahama huku na kule hususan kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo na kusaka hifadhi nchi  jirani.

Nuru ikiwa angalau inataka kuchomoza gizani, ghafla Oktoba 9 yaani jana Jumatano, mashambulizi mapya kutoka angani  yanakumba raia na kusababisha waanze kukimbia tena huku na kule.

Kufuatia hatua hiyo, Kamisheni huru ya kimataifa ya uchunguzi dhidi ya Syria imetoa taarifa yake ikisema mashambulizi zaidi yanaweza kuleta sintofahamu kwa raia huko mipakani wanakosaka kukimbilia nchi jirani na pia kuharibu miundombinu muhimu ya kiraia na ile inayotumika kusambaza huduma za kibinadamu.

“Raia wengi wamefurushwa mara kadhaa kutokana na mzozo huo au kuwa wamelazimika kuishi chini ya utawala wa kikundi cha kigaidi cha ISIL,” imesema Kamisheni hiyo ikiongeza kuwa zaidi ya wakimbizi 100,000 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wanaishi kwenye kambi za muda ikiwemo huko Al-Hol, Al-Roj, na Ain-Issa, huku huduma za kijamii zikiwa ni za kusuasua, mipango ya kusaidia makundi hatarishi ikiwa haipo.

UNHCR nayo yazungumza

Mashambulizi hayo mapya  yamesababisha shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR kusema kuwa mzozo huo kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo kunaongeza machungu zaidi kwa wananchi ambao tayari wameshafurushwa huku na kule na kusababisha janga la wakimbizi Syria kuwa janga kubwa zaidi duniani.

“Makumi ya maelfu ya raia wanakimbia mapigano ili kusaka maeneo salama,” amesema Kamishna Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi kupitia taarifa iliyotolewa leo Geneva, Uswisi akiongeza kuwa hali ya wale walionaswa kwenye mapigano ni mbaya na itakuwa mbaya zaidi kutokana na viwango vya joto kushuka wakati  huu majira ya baridi yanakaribia.”

Bwana Grandi ametoa wito kwa pande kinzani kwenye mzozo huo wa Syria wazingatie sheria za kimataifa za haki za binadamu, ikiwemo kuhakikisha mashirika ya misaada yanafikisha shehena za usaidizi kwa wahusika.

UNICEF nayo yapaza sauti

Kwa upande wake shirika la kuhudumia watoto duniani,  UNICEF limesema lina wasiwasi mkubwa na kinachoendelea kaskazini-mashariki mwa Syria na kusihi pande husika zilinde watoto na miundombinu ya kijamii inayotegemewa kufikishia misaada wahitaji.

Taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo jijini New York, Marekani imesema, “mashambulizi zaidi ya kijeshi kaskazini-mashariki mwa Syria yanaweza kuathiri zaidi vibaya uwezo wa mashirika ya kibinadamu kufikisha misaada kwa watoto walio hatarini zaidi.”

UNICEF imeongeza kuwa,  “kama tulivyosema tena na tena, suluhu pekee ya mgogoro huu ni kupitia njia za kisiasa. Pande zote lazima zijizuie kutumia nguvu.”

Baada ya miaka minane ya mzozo nchini Syria, taifa hilo linasalia kuwa janga kubwa zaidi la wakimbizi duniani ikiwa na wakimbizi zaidi ya milioni 6.2 ambapo wakimbizi milioni 5.6 kati yao hao wanaishi ugenini, Uturuki ikiwa ndio inahifadhi wasyria wengi zaidi idadi yao ikiwa milioni 3.6.