Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Upepo wa mafanikio unaovuma DRC unategemea juhudi zaidi za kuimarisha dola- Zerrougui

Mmoja wa askari wanawake kutoka Afrika Kusini anayehudumu kwenye ujumbe wa kulinda amani wa UN huko DRC, MONUSCO akiwa lindoni
MONUSCO
Mmoja wa askari wanawake kutoka Afrika Kusini anayehudumu kwenye ujumbe wa kulinda amani wa UN huko DRC, MONUSCO akiwa lindoni

Upepo wa mafanikio unaovuma DRC unategemea juhudi zaidi za kuimarisha dola- Zerrougui

Amani na Usalama

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo wamejulishwa ya kwamba pamoja na hatua zozote zinazochukuliwa kukabiliana na vitisho vya usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, hatua za makusudi lazima zichukuliwe kuimarisha vyombo vya dola ikiwemo mahakama na jeshi.

Ushauri huo umetolewa na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, Leila Zerrougui wakati akihutubia Baraza hilo kwa njia ya video kuhusu hali nchini  humo kwa kuzingatia ripoti ya Katibu Mkuu iliyokabidhiwa wajumbe.

Bi. Zerrougui amesema, “naamini kwa dhati kuwa pamoj na kukabili vitisho vya usalama kwa njia ya kijeshi, hatua zaidi zinatakiwa kuimarisha majukumu ya msingi ya dola  ikiwemo iwe na jeshi lenye ueledi, sekta ya usalama na uwezeshaji wa mahakama na hii itawezesha serikali kushughulikia vyema yenyewe hivyo vitisho.”

Ripoti hiyo ya Katibu Mkuu ilikuwa inamulika utendaji wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani DRC, MONUSCO, ujumbe ambao unaongozwa pia na Bi. Zerrougui.

Ni kwa mantiki hiyo amesema kuwa, “pamoja na kushughulikia vyanzo vya mizozo inayoendelea, MONUSCO unapatia msisitizo usaidizi kwa serikali katika kuhamasisha maridhiano na mashauriano kuanzia ngazi ya taifa hadi mashinani na kuchukua hatua dhidi ya vitendo vinavyochochea chuki baina ya makabila, na ujumbe huo unafanya hivyo kupitia mikakati inayolenga kukabili kauli za chuki.”

Mapigano ya kikabila,  ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu pamoja na mashambulizi kutoka vikundi vilivyojihami yamekuwa chanzo cha watu kukimbia makazi yao kwenye majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri.

Doria kutoka juu ya kifaru ikifanywa na walinda amani wa kike kutoka Afrika Kusini walio kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO
MONUSCO
Doria kutoka juu ya kifaru ikifanywa na walinda amani wa kike kutoka Afrika Kusini walio kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO

Ripoti ya Katibu Mkuu inaonesha kuwa idadi kubwa ya vikundi vilivyojihami, iwe vya kitaifa au vya kigeni vikiwemo Allied Democratic Forces, ADF, Nduma défense du CongoRénové NDC-R na Forces démocratiques de libération du Rwanda, FDLR, vimeendelea kuongeza machungu kwa raia ambao tayari wanakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu.

Bi. Zerrougui akatolea mfano tukio lililomtia huzuni zaidi kuwa ni ukatili dhidi ya raia. “Mauaji  ya hivi karibuni na ukatwaji viungo vya raia 14, wakiwemo watoto 11 huko Bukatsele jimbo la Ituri na visa vya ukeketaji huko eneo la Fizi jimboni Kivu Kusini havikubaliki na vinachukiza na hivyo tunachukua kila hatua kuhakikisha watekelezaji wanakamatwa na wanawajibishwa.”

Hata hivyo mkuu huyo wa MONUSCO ameonesha kutiwa matumaini yake na mchakato unaoendelea wa kuhusisha kikundi kilichojihami huko Ituri kiitwacho Force de Résistance Patriotique de I'Ituri, akisema mchakato huo unadhihirisha juhudi za kuhakikisha mazingira salama yenye utashi wa kisiasa na ushiriki wa jamii unaweza kuzaa  matunda.

Hivi sasa zaidi ya watu zaidi ya 900 waliokuwa wamejihami wako kwenye kambi wakisubiri makubaliano ya amani yanayotarajiw kukamilishwa baadaye mwaka huu.

“Kando ya mchakato huu, ujumuishwaji wa wafuasi wa zamani wa vikundi vilivyojihami kufuatia wimbi la watu kujisalimisha kwa hiari mapema mwaka huu wa 2019 bado ni kazi kubwa. Naamini kwa dhati kuwa kitendo hiki kitakuwa na athari chanya kwenye utulivu wa taifa hili,” amesema Bi. Zerrougui.

Amesisitiza utayari wa MONUSCO katika kusaidia serikali  ya DRC kulinda raia na kusongesha utulivu pamoja na kuimarisha taasisi muhimu huku akiomba wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa waendelee kuunga mkono juhudi hizo.