Surua DRC ni tishio kuliko Ebola, idadi ya vifo sasa ni 4,000- UNICEF

9 Oktoba 2019

Mlipuko wa ugonjwa wa Surua nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC umeendelea kuwa tishio wakati huu ambapo idadi ya vifo imefikia 4,000 na hivyo kulazimu mashirika ya Umoja wa Mataifa kuendelea kuwapatia chanjo watoto zaidi na kupeleka dawa za kuokoa maisha.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kupitia taarifa yake iliyotolewa leo mijini New York, Marekani na Kinshasa, DRC inasema idadi hiyo ya vifo ni tangu mwezi Januari mwaka huu kati ya wagonjwa 203,179 walioripotiwa kwenye majimbo yote 26 ya taifa hilo.

Cha kusikitisha zaidi, asilimia 74 ya wagonjwa hao wa surua ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano  na mbaya zaidi takribani asilimia 90ya vifo ni watoto wa umri huo.

Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC, Edouard Beigbeder amesema idadi  ya wagonjwa wa surua nchini humo mwaka huu ni mara tatu zaidi ya wagonjwa walioripotiwa mwaka 2018 akisema kuwa surua umekuwa ugonjwa hatari zaidi kuliko Ebola ambayo tangu mwezi Agosti mwaka jana hadi leo hii umesababisha vifo vya watu 2,143.

Bwana Beigbeder amesema, “tunakabili mlipuko wa Surua kwa njia mbili, kwa kuzuia maambukizi na kuzuia vifo. Kwa ushirikiano na serikali na wadau wetu wakuu, tunaongeza kasi ya utoaji wa chanjo kwa watoto na wakati  huo huo tunazipatia kliniki dawa kutibu dalili za ugonjwa na kuongeza fursa ya walioambukizwa kuweza kuishi.”

Tayari wiki hii pekee, vikasha 1,111 zaidi vya tiba vimesambazwa kwenye vituo vya afya katika maeneo hatari zaidi kukumbwa na surua ambapo vikasha hivyo vina dawa aina za viuavijasumu, maji yenye chumvi, Vitamin A, dawa za kuzuia maumivu na vifaa vingine kwa ajili ya zaidi ya watu 111,000 walioambukizwa ugonjwa huo hatari.

Katika mwaka mmoja uliopita, UNICEF imesambaza zaidi ya dozi milioni 8.6 za chanjo dhidi ya surua ambapo shirika hilo liliongoza kampeni ya chanjo kwenye majimbo manane yaliyokumbwa zaidi na surua na kupatia chanjo watoto zaidi ya milioni 1.4.

Kampeni ya hivi karibuni zaidi ni ya kwenye jimbo la Kasai Kati ambako zaidi ya watoto 210,000 walipatiwa chanjo.

Hata hivyo mwakilishi huyo wa UNICEF nchini DRC amesema, “tunakabiliwa na hali tete kwa sababu mamilioni ya watoto wa DRC wanakosa mzunguko wa chanjo na hawawezi kupata huduma za afya pindi wanapougua. Na zaidi ya hapo mfumo dhaifu wa chanjo, ukosefu wa usalama, tabia ya jamii kutoamini chanjo na watoa chanjo sambamba na changamoto za miundombinu vinasababisha watoto wengi wasio na chanjo kuwa hatarini kuambukizwa surua.”

Kwa mujibu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO, kinachopendekezwa ni dozi mbili za chanjo dhidi ya surua na takribani asilimia 95 ya wananchi w DRC wanapaswa kupatiwa chanjo ili kujenga kinga ya mwili na kuzuia milipuko.

Nchini DRC, kwa mwaka 2018, chanjo dhidi ya surua ilifikia asilimia 57 tu ya wananchi wote.

“Iwapo tunataka kuepusha milipuko mibaya zaidi kama hii ya surua siku za usoni, lazima kunapaswa kuwepo uwekezaji wa hali ya juu katika kuimarisha mpango wa chanjo wa kitaifa, DRC na kushughulikia changamoto za ufikiaji eneo kubwa zaidi,” amesema Bwana Beigbeder.

Tayari serikali ya DRC inajiandaa kuzindua awamu ya pili ya kampeni ya chanjo tarehe 22 mwezi huu wa Oktoba, ambayo ina lengo kupatia chanjo dhidi surua watoto wenye umri kuanzia miezi 6 hadi miaka mitano katika majimbo yote 26.

Kampeni hii inaungwa mkono na wadau wengi ikiwemo UNICEF ambayo inatoa msaada wa kiufundi katika ngazi ya kitaifa, majimbo hadi mashinani kwa kusambaza canjo na kusaidia kuendesha kampeni ya uhamasishaji.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud