Ghasia Haiti zimeathiri kazi zetu:WFP

8 Oktoba 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP limesema katika wiki tatu zilizopita hali ya usalama nchi Haitri imeathiri kwa kiasi kikubwa kazi za shirika hilo na mahisrika mengine ya kibinadamu kuweza kuwafikia  maelfu ya watu wanaohitaji msaada.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi hii leo amesema moja ya shughuli za muhimu zilizoathirika ni “mpango wa WFP wa mlo mashuleni ambao unachukuliwa kama moja ya miradi mikubwa ya kuokoa maisha nchini Haiti. WFP inalenga kugawa chakula mashuleni kwa watoto 300,000 kila siku nchini Haiti , lakini usambazaji wa chakula umesitishwa kwa muda kutokana na kutokuwepo na usalama.”

Ameongeza kuwa hata hivyo tarehe 6 wiki hii kwa mara ya kwanza katika kipindi cha wiki tatu WFP imeweza kufikisha chakula katika shule 14 ambazo ni sehemu ya mradi huo kitakachowasaidia watoto 4000, na licha ya mafanikio hayo katika shule 14 shule nyingine nyingi nchini Haiti bado zimefungwa na hazijaweza kupokea mgao wa chakula wanaouhitaji ili kutoa chakula kila siku kwa watoto. Shirika hilo pia limeahirisha usambazaji wa msaada kupitia mpango wa fedha taslim ambao uliwekwa kwa ajili ya watu wanaokabiliwa na kutokuwa na uhakika wa chakula.

WFP inasema hali hii “inaathiri jamii zisizojiweza kabisa nchini Haiti ambazo zimekuwa zikitegemea msaada ili kuweza kulisha familia zao.”

Mwanzoni mwa mwaka huu watu milioni 2.6 walikuwa hawana uhakika wa chakula nchini Haiti na endapo hali ya sasa itaendelea WFP inasema maelfu ya watu ambao taryari wameshaathirika na kutokuwa na uhakika wa chakula hali yao itakuwa mbaya zaidi hasa kutokana pia na msaada wa chakula kushindwa kuwafikia.

WFP inawachagiza wadau wote kuheshimu misingi ya kiutu na ubinadamu, huruma , wema na kutoegemea upande wowote ili waruhusu wahudumu wa misaada ya kibinadamu kutoa msaada kwa maelfu ya watu wanaouhitaji msaada huo haraka.

Hata hivyo shitrika hilo limesema liko tayari kuandaa na kuendesha ugawaji wa chakula kila wakati hali ya usalama itakapotengamaa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud