Skip to main content

UN yakabiliwa na ukata, Katibu Mkuu asihi nchi zilipe michango yao

Jengo la Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani
UN Photo/Rick Bajornas)
Jengo la Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani

UN yakabiliwa na ukata, Katibu Mkuu asihi nchi zilipe michango yao

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo ameziandikia barua nchi wanachama kuhusu ukata mbaya zaidi kuwahi kukabili chombo hicho chenye wanachama 193 kwa karibu muongo mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari   hii leo mjini New York, Marekani, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amenukuu barua hiyo ya Guterres ikisema kuwa, “shirika hili liko hatarini kukomba akiba zake zote ifikapo mwishoni mwa mwezi hu una kushindwa kulipa wafanyakazi na watoa huduma.”

Akisisitiza wajibu wa nchi wanachama kwa mujibu wa Katiba iliyoanzisha Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu ameshukuru nchi zilizolipa michango yao ambazo sasa ni 131 na kusihi zile ambazo hazijalipa kufanya hivyo haraka na kwa ukamilifu akisema kuwa, “hii ndio njia pekee ya kuepusha kutokulipa ambako kunaweza kuathiri operesheni zetu ulimwenguni kote.”

Katibu Mkuu amesihi serikali zishughulikie chanzo cha hali ya sasa ya ukata na zikubaliane juu ya mikakati ya kuhakikisha hali ya kifedha ya Umoja wa Mataifa inakuwa ni nzuri.

Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi uliopita, nchi wanachama zilikuwa zimelipa asilimia 70 tu ya fedha kwa ajili ya bajeti ya kawaida ya Umoja wa Mataifa, ikilinganishwa na asilimia 78 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Hata hivyo amesema tayari sekretarieti anayoongoza ya Umoja wa Mataifa imeshachukua hatua za makusudi kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu kuhakikisha kuwa matumizi yake inaendana na kiwango cha fedha kilichopo.

Ametaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuangalia upya masuala ya ajira kwa kuzingatia fedha zinazotarajiwa kupatikana. “Iwapo tusingalichukua hatua za matumizi tangu mwanzoni mwa mwaka huu, pengo la fedha kwa mwezi huu wa Oktoba lingalifikia dola milioni 600 na Umoja wa Mataifa usingalikuwa na uwezo wa kuendesha ufunguzi wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu na vikao vya ngazi ya juu mwezi uliopita. Hadi leo hii, tumeweza kuepuka matukio makuu ya kukwamisha operesheni zetu.,” amesema Guterres.

Katibu Mkuu wa UN António Guterres(katikati) akizungumza kwenye mkutano wa Kamati ya 5 ya Baraza Kuu la UN kuhusu mpango pendekezwa wa bajeti. (08 Oktoba 2019)
UN Photo/Eskinder Debebe)
Katibu Mkuu wa UN António Guterres(katikati) akizungumza kwenye mkutano wa Kamati ya 5 ya Baraza Kuu la UN kuhusu mpango pendekezwa wa bajeti. (08 Oktoba 2019)

Hatua zaidi kuchukuliwa kukabiliana na ukata

Hata hivyo amesema hatua hizo bado hazitoshi na kwamba, “Sekretarieti inaweza kushindwa kulipa mishahara na malipo ya bidhaa na huduma ifikapo mwishoni mwa mwezi Novemba iwapo nchi wanachama hazitalipa malimbikizo yao yote.”

Kwa mujibu wa Dujarric, tayari Katibu Mkuu ametangaza hatua zaidi za kuchukua haraka iwezekanavyo ili kuhakikisha hali ya fedha  inakuwa nzuri, ikiwemo, kupunguza safari rasmi, kusogeza mbele manunuzi ya bidhaa na huduma, kusitisha matukio ambayo yangepaswa kufanyika nje ya saa rasmi za kazi kwenye  makao makuu. Halikadhalika, mikutano inaweza kuahirishwa au huduma zikapangwa upya na kwamba Katibu Mkuu anafikiria hatua zaidi.

Bwana Guterres amenukuliwa pia akisema kuwa tatizo la ukata limekuwa likitokea mara kwa mara na linakwamisha uwezo wa Sekretarieti kutekeleza wajibu wake. “Badala yake tunalazimika kutekelza majukumu kwa kuangalia uwezo wa fedha na hivyo kudumaza utekelezaji wa majukumu yaliyopitishwa.”

Kwa mujibu wa Dujarric, Katibu Mkuu amewajulisha wafanyakazi kuhusu hali ya fedha ya shirika.

UN yahitaji dola bilioni 2.87 kwa mwaka 2002

Wakati huo huo, Katibu Mkuu amewasilisha mbele ya Kamati ya 5 ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mpango wa bajeti kwa mwaka 2020, ikiwa ni mpango wa kwanza wa bajeti yam waka ikilinganishwa na bajeti za awali zilizokuwa ni za miaka miwili miwili.

Mpango huo  unahitaji dola bilioni 2.87 kwa ajili ya Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa iweze kufanya kazi  yake ambapo Guterres amesema kiwango hicho si tofauti sana na bajeti ya m mwaka 2019.

Katibu Mkuu ametumia hotuba yake pia kuwaeleza wajumbe kuhusu ukata unaokabili shirika na hatua ambazo tayari ameshachukua kukabiliana nayo huku akisihi nchi wanachama zilipe michango yao kwa ukamilifu.

Amesema michango hiyo ni muhimu ili kutekeleza majukumu ya Umoja wa Mataifa kwa kuzingatia changamoto kubwa zinazokabili dunia hivi sasa kuanzia amani na usalama, mabadiliko ya tabianchi na haki za binadamu.

Bwana Guterres amewahakikishia kuwa tayari kuna mifumo ya uwazi katika matumizi ya fedha na tayari mikakati hiyo imeanza kufanya kazi na kuzaa matunda.

Chemchem hii iliyopo nje ya jengo la makao makuu ya UN jijini New York, Marekani nayo itazimwa ili kuokoa fedha
UN Photo/Rick Bajornas)
Chemchem hii iliyopo nje ya jengo la makao makuu ya UN jijini New York, Marekani nayo itazimwa ili kuokoa fedha

Viyoyozi na lifti kuzimwa ili kuokoa fedha- Pollard

Kutokana na ukata unaokumba shirika, Mkuu wa Idara ya Menejimenti ya Umoja wa Mataifa, Catherine Pollard amezungumza na waandishi wa habari na kuelezea hatua thabiti ambazo zinachukuliwa ili kuhakikisha operesheni zinaendelea.

“Kwa mwaka wa pili mfululizo, tumetumia fedha zote za akiba ya  bajeti ya kawaida licha ya hatua madhubuti ambazo tuliweka ili kupunguza matumizi na kwenda sambamba na akiba yetu. Kutakuwepo na uchelewashwaji wa nyaraka. Mathalani tumesitisha uchapishaji wa mikataba na machapisho, tunapunguza safari rasmi za wafanyakazi na zitakazofanyika ni zile za ulazime tu,” amesema Bi. Pollard.

Ameongeza kuwa hawataweza kuwa wenyeji wa matukio kama vile hafla kabla ya saa mbili asubuhi au baada ya saa 12 jioni. “Viyoyozi kwa ajili ya joto au baridi vitazimwa ili kupunguza gharama, halikadhalika lifti katika baadhi ya ghorofa zitapunguzwa pamoja na chemchem iliyoko nje ya jengo nayo  itazimwa,´amesema Mkuu huyo wa Menejimenti Umoja wa Mataifa.

Bi. Pollard ameongeza kuwa tayari wanaendelea kuwasiliana na  nchi wanachama ambazo bado hazijalipa ili ziweze kufanya hivyo.

Ameweka bayana kuwa kinachohitajika ni kati ya dola milioni 200 hadi milioni 250 ambazo ni pengo litokanalo na kasi ndogo ya malipo.

Tayari Bi. Pollard amehutubia pia kamati ya tano ya Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa ambayo ndiyo inahusika na masuala ya bajeti. 

Halikadhalika alikuwa na kikao na kamati ya ushauri wa masuala ya bajeti ya Umoja wa Mataifa ambako alijibu maswali kuhusiana na sakata la ukata linalokumba bajeti ya kawaida ya Umoja wa Mataifa inayofikia ukomo tarehe 31 Disemba mwaka huu wa 2019.

Naye Mdhibiti Mkuu wa hesabu za UN, Chandramouli Ramanathan amesema kuwa, “tunajaribu kuhakikisha kuwa tuna fedha za kutosha kulipia malipo ya huduma kwa mwezi Oktoba na  Novemba na tunatarajia hali itakuwa imeshakuwa nzuri ifikapo wakati huo.”

Amesema hivi sasa anajaribu kutunza kila senti apatayo na kwamba, hadi hii leo, nchi wanachama hazijalipa jumla ya dola bilioni 1.4 ambazo ni mchango wao kwa Umoja wa Mataifa. Miongoni mwao ni Marekani ambayo ndio hutoa mchango mkubwa zaidi na inadaiwa takribani dola bilioni 1.

(Video chini ni Catherine Pollard akihutubia kikao cha Kamati ya Tano ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 11 Oktoba 2019)

 

 

 

Pamoja na kufanya vikao na kamati mbalimbali bila kusahau kuwa na mkutano na waandishi wa habari, Bi.Pollard pia alishatoa taarifa kuhusu hali halisi ya bajeti ya kawaida ya Umoja wa  Mataifa.