Nimejitolea kukomesha ajira kwa watoto Uganda sababu nimeipitia:Namirembe

8 Oktoba 2019

Wahenga walisema siri ya mtungi aijuaye kata na uchungu wa ajira ya mtoto anaujua mtoto aliyeipitia, kauli hiyo imetolewa na Molly Namirembe mwanaharakati wa kupambana na ajira ya watoto nchini Uganda ambaye yeye mwenyewe alipitia madhila hayo na jinamizi lake linamtesa hadi sasa. Kupitia mradi wa SCREAM unaosaidiwa na shirika la kazi duniani ILO Namirembe amedhamiria kupambana na ajira hiyo nchini mwake. 

Molly Namirembe ambaye jina lake Namirembe likimaanisha amani alipohojiwa na ILO amesema amejitoa kimasomaso katika mradi huo unaopigania haki za watoto kupitia elimu, sanaa na vyombo vya Habari kama mkufunzi. Yeye na dada yake waliteseka sana wakifanya kazi katika mashamba ya chai kupitia ajira ya watoto, “ilihusisha maumivu makubwa kwanza tulifanya kazi kwa sasa nyingi tulikuwa tunaamka saa 12 asubuhi na kufanya kazi hadi jioni , hakuna kupumzika na wakati mwingine bila kula chochote na haya yote yalitokea baada ya wazazi wetu kufa. Mamama yangu alikufa nikiwa na umri wa miaka 11 na dada yangu miaka 14.”

Mbali ya kutumikishwa ilibidi wajilee wenyewe, “ilikuwa vigumu sana kukabilia hali hiyo, na tuliishi katika familia inayoongozwa na mtoto kwa takriban miaka 3, tukijuhudumia wenyewe, kitu pekee tulichojua ni kufanya kazi katika mashamba ya chai kwani hiyo ndio kazi aliyokuwa akifanya mama yetu.”

Pamoja na zahma zote hizo ambayo hadi leo zimemwacha Molly na maumivu ya mgongo na dada yake kutosoma kabisa kwani ilibidi awe mama wa wadogo zake akiwa na miaka 14 tu, Molly hakukata tamaa ya kutimiza ndoto yake ya kuwasaidia watoto wengine wanaopitia janga hilo na anasema cha kusikitisha zaidi,“watu walikuwa wanatupongeza kwa kufanya kazi kwa bidi, kwa kujitimizia wahitaji yetu wenyewe, hawakujali mateso tuliyokuwa tukiyapitia, hawakujali kuhusu mustakbali wetu, na kwangu mimi ninapowaona watoto wengine wanapitia nilichopitia inanihuzunisha , inanifanya nitake kulia na ndio maana najitolea maisha yangu yote kuwalinda wengine dhidi ya ajira ya watoto.”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter