Taka zaweza kuwa mali kubwa zikitumika ipasavyo:UN

7 Oktoba 2019

Taka zinaweza kuleta madhara makubwa kwa afya ya umma, mazingira na hali ya hewa , lakini katika zama hizi sayansi, teknolojia na ubunifu wa hali ya juu vinaweza kuleta suluhu ya gharama nafuu katika changamoto hiyo ya taka na kuisaidia miji na jamii kuziona taka kama ni fursa ya biashara . Huu ndio ujumbe wa maadhimisho ya siku ya makazi duniani ambayo kila mwaka hufanyika Oktoba 7.

Kaulimbiu ya mwaka huu ya siku ya makazi imejikita katika udhibiti wa taka lakini pia kuzitumia kama fursa ya kipato na kiuchumi.

Katika ujumbe wake maalum wa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, “ni lazima tupunguze kiwango cha taka tunachozalisha na wakati huohuo tuanze kuziona taka hizo kama ni rasilimali ya thamani ambayo inaweza kutumiwa tena na tena ikiwemo katika kuzalisha nishati.”

Sanjari na maazimisho ya leo shirika la Umoja wa Mataifa la makazi UN-HABITAT limezindua kampeni ijulikanayo kama “Waste Wise Cities” ili kushughulikia shangamoto zinazoongezeka za kushughulikia tatizo la taka.

Na kama sehemu ya kampeni hiyo miji inaalikwa kuthibitisha ahadi zao za kutekeleza mikakati iliyoafikiwa ambayo ni pamoja na kutathimini kiwango na aina ya taka, kuboresha ukusanyaji wa taka, kuhakikisha mazingira ya miji ni salama na kutekeleza miradi ya kubadili taka kuwa nishati.

Guterres amesema kampeni hiyo imebaini kwamba suala la taka linatumia bajeti kubwa ya miji na kwamba udhibiti wa taka haufadhiliwi kiasi cha kutosha . Lakini “teknolojia za kisasa zinaweza kutoa majibu ya suala hilo na kwa gharama nafuu ya jinsi ya kusafisha miji yetu.” Teknolojia hizo ni pamoja na akili bandia (AI)ambayo ikitumika kwa pamoja na teknolojia zingine inaweza kusaidia kurejelea matumizi ya vitu kwa ufanisi zaidi. Suluhu nyingine ni kama vifungashio salama vinavyohjali mazingira, kutumia teknolojia kupunguza kiasi cha chakula kinachotupwa na teknolojia mpya bunifu ambayzo zinaweza kubadili taka kuwa nishati endelevu na mbolea.

UN-HABITAT imesema teknolojia pia inatoa fursa kwa miji mipya na inayokuwa kwa kasi katika nchi zinazoendelea kuipita miji ya zamani kwa kutumia fursa ya teknolojia ya sasa na kuepuka njia za zamani ambazo hazina ufanisi wa kutosha.

Kwa kutumia vyema nyenzo zilizopo za kisasa amesema Katibu Mkuu kunaweza kusaidia kujenga mustakabali bora , uliopangika na unaoweza kudhibitiwa wa miji yetu ambao untachagiza ukuaji jumuishi na maendeleo yasiyochafua mazingira.

Hata hivyo Umoja wa Mataifa unasisitiza kwamba nyenzo hizo mpya ni lazima ziende sambasamba na será bora, kuzisaidia nchi kutotumbukia katika janga lingine na kupunguza gharama za kiuchumi na kijamii za masuala ya teknolojia.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter