Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafanikio ya mradi wa TASAF Tanzania wasababisha Benki ya Dunia kufadhili awamu ya II

Uwezeshaji wa jamii ili kusongesha maendeleo endelevu ikiwemo sekta ya kilimo ni moja ya mada katika mkutano wa kuimarisha ubia kati ya UN na AU
©FAO/Amos Gumulira
Uwezeshaji wa jamii ili kusongesha maendeleo endelevu ikiwemo sekta ya kilimo ni moja ya mada katika mkutano wa kuimarisha ubia kati ya UN na AU

Mafanikio ya mradi wa TASAF Tanzania wasababisha Benki ya Dunia kufadhili awamu ya II

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchini Tanzania, Benki ya Dunia hii leo imetiliana saini na serikali  ya taifa hilo la Afrika Mashariki mkataba mkopo nafuu wa dola milioni 540 za kimarekani sawa na shilingi trilioni 1.04 za kitanzania.

Makubaliano hayo yametiwa saini kati ya Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Bella Bird na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Doto James na fedha zitatumika kwenye awamu ya pili ya mradi wa kunusuru kaya, PSSN unaotekelezwa na mfuko wa maendeleo ya jamii, TASAF.

Mkopo huo nafuu ulioidhinishwa na bodi ya Benki ya Dunia tarehe 12 mwezi uliopita wa Septemba, unasaka kuimarisha lishe bora na kuinua kipato huku ukiongeza mahudhurio ya watoto shule ya msingi na kumaliza masomo, sambamba na kupata huduma za afya.

Mwakilishi huyo wa Benki  ya Dunia akizungumza baada ya utiaji saini amenukuu takwimu za tathmini  ya kati ya mradi huo akisema kuwa, “TASAF imekuwa na mafanikio makubwa katika kufikia wale walio maskini zaidi nchini Tanzania. Zaidi ya asilimia 60 ya wanufaika wa mradi huu wako kwenye kundi la asilimia 20 ya watu maskini zaidi kwa vigezo vya matumizi.”

Amefafanua kuwa kaya zinazopokea fedha kupitia mradi huo wa kunusuru kaya maskini zimepunguza umaskini kwa asilimia 10 na kuongeza kwa asilimia 20 kiwango chao cha matumizi kwa mwezi ikilinganishwa na kaya ambazo hazikupata msaada huo.

Tweet URL

Bi. Bird ameenda mbali zaidi akisema kuwa, mabadiliko yameonekana pia kwenye idadi ya watoto wanaoandikishwa shuleni, kiwango cha kujua kusoma na kuandika, wanawake kufika katika huduma za afya ya mama na mtoto pamoja na huduma za afya kwa mtoto bila kusahau “bima ya afya, uhakika wa kupata chakula na umiliki wa mali,” jambo ambalo amesema ni muhimu katika kutokomeza umaskini.

Akizungumza kwenye tukio hilo, Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Fedha na Mipango amesema, “tunatia saini makubaliano haya ya mkopo wa fedha kuashiria kuanza kwa awamu ya pili ya PSSN. Licha ya mafanikio, bado umaskini unasalia changamoto. Naahidi azma ya serikali yangu katika kufanikisha awamu ya pili ili ifikie malengo yake.”

Bwana James ameshukuru Benki ya Dunia kwa hatua hiyo akisema, “kwa niaba ya serikali ya Tanzania, napenda kutoa shukrani zangu kwa Benki ya Dunia kwa kuendelea kusaidia miradi ya maendeleo nchini mwetu. Awamu ya majaribio ya TASAF ilinufaisha raia milioni 7.3 katika wilaya 40. Awamu ya kwanza ya PSSN ilifikia wanufaika milioni 18.6 katika wilaya 126.”

Benki ya Dunia imeshukuru wadau wake, wakiwemo DFID, Norway, SIDA, UNICEF, WFP, UN-Women, taasisi ya Gates akisema,  “kwa pamoja tunatumai kuendelea kuboresha maisha ya watanzania na tunasubiri kwa hamu kufanikisha awamu hii mpya.”