Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ualimu ni wito wangu popote nitafundisha- Mkimbizi Koat Reath

Koat Reath, mkimbizi kutoka Sudan Kusini sasa anaishi Ethiopia ambako pia anafundisha akiamini kuwa elimu ni msingi wa mustakabali wenye nuru kwa taifa lake.
UN News
Koat Reath, mkimbizi kutoka Sudan Kusini sasa anaishi Ethiopia ambako pia anafundisha akiamini kuwa elimu ni msingi wa mustakabali wenye nuru kwa taifa lake.

Ualimu ni wito wangu popote nitafundisha- Mkimbizi Koat Reath

Utamaduni na Elimu

Ualimu ukiwa ni wito wako popote utafundisha , hiyo ni kauli ya mkimbizi kutoka Sudan Kusini ambaye pia ni mwalimu kwa sasa yuko ukimbizini nchini Ethiopia anakoendeleza wito wake wa ualimu kwa watoto wakimbizi. Amina Hassan na taarifa zaidi

Darasani kwenye kambi ya Jewi nchini Ethiopia, watoto wakiimba kwa shangwe na mwalimu wao kama sehemu ya masomo. Mwalimu Koat Reath alikimbia machafuko Sudan kusini na bado anaamini elimu ndio ufunguo wa mustakbali bora nyumbani alikotoka na anataka kuhakikisha watoto, vijana na wazee wanashiriki kujenga mustakbali huo popote walipo

Mwalimu Reath anasema kwamba “napenda kufundisha kwa sababu nataka kuwasukuma kizazi hiki kichanga kuwa watoto bora siku za usoni (…Natts…)  Nawafundisha kwa kutumia lugha mbalimbali na nyinmbo tofauti. Nawafundisha kwa Kinuer na Kiingereza kidogo ili wafahamu.”

 Darasa limefurika, na hakuna vitabu vya kutosha, lakini Koat Reath hakati tamaa wala kulalamika. Vivyo hivyo baadhi ya wanafunzi wake kama Nyamani Pur wanaopenda kazi yake wanafunguka, “ninapenda anavyofundisha, na anafurahisha sana napenda mbinu zake.”

 Mwalimu Koat Reath mwenye umri wa miaka 41 anasema licha ya changamoto zote zinazowakabili wanafunzi ikiwemo kukosa viatu, msongo wa mawazo, kutopata chakula cha kutosha na hata vifaa, anachoka kuyashuhudia madhila hayo lakini hakati tamaa kwani anaandaa kizazi kijacho akisema kwamba, “nafundisha watoto hawa kuwa Daktari, Rais na rubani, hilo ndilo jukumu langu  la kujitolea kufundisha watoto hawa ili kujenga mustakbali bora Sudan Kusini, na kufanya kitu kizuri.”

Mwalimu Reath ni miongoni mwa zaidi ya wakimbizi milioni 2 kutoka Sudan Kusini  na zaidi ya asilimia 60 ya wakimbizi hao ni watoto. Yeye hujitolea kufundisha watoto asubuhi na watu wazima jioni kila siku.