UN na FIFA waingia ubia kuhamasisha afya kupitia michezo

4 Oktoba 2019

Katika hafla iliyofanyika hii leo mjini Geneva Uswisi, shirika la afya duniani WHO na shirikisho la soka duniani FIFA, wametangaza ubia katika kukuza uelewa wa faida za kuishi maisha yenye afya.

Kwa kutia saini mkataba wa makubaliano katika makao makuu ya WHO, mashirika yote mawili yameweka ahadi ya miaka minne ya ushirikiano katika kuhamasisha maisha ya kiafya kupitia michezo kimataifa, lakini pia kupitia michezo kuwa na uwezo wa kusambaza ujumbe kwenda kwa idadi kubwa ya watu.

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhom Ghebreyesus wakati wa uzinduzi wa ushirikiano huo amesema, “nusu ya watu wote ulimwenguni walitizama kombe la dunia mwaka 2018. Hii inamaanisha kuwa kuna uwezekano mkubwa kwetu kuungana kuwaafikishia taarifa mabilioni ya watu za kuwasaidia kuishi maisha marefu na yenye afya.”

Katika hafla hiyo, FIFA imewakilishwa na Rais wa shirikisho hilo lilnalosimamia kwa ngazi ya juu mchezo wa soka ulimwenguni Bwana Gianni Infantino ambaye ameeleza kuridhishwa kwake na ushirikiano wa mashirika hayo mawili. Bwana Infatino amesema, “mpira wa miguu ni wa kipekee, ni lugha ya dunia nzima na tunataka kutumia jukwaa yetu na mtandao wetu kuunga mkono mpango wa kiafya na kukuza maisha bora kote ulimwenguni.”

Sigara inapigwa kadi nyekundu

Juhudi za kuwashawishi mashabiki wa soka kuachana na uvutaji wa sigara itakuwa sehemu ya ushirikiano huu kati ya WHO na FIFA, ambao tayari wana ushirikiano katika kampeni ya kupambana na uvutaji wa sigara ikiwemo katika kombe la dunia la mwaka 2018.

WHO itafanya kazi na FIFA kuhakikisha inaweka mazingira ya kutokuwepo kwa sigara katika matukio yatakayoandaliwa na shirikisho hilo la soka, kuhamasisha mashirikisho ya soka ya mataifa kuitekeleza sera ya matukio bila sigara na pia kuwapa FIFA ushauri wa kitaalamu katika masuala kadhaa ya kiafya ikiwemo usafi na kudhibiti magonjwa.

Kwa kipindi cha miaka miaka minne, programu za pamoja na mipango ya pamoja zinayohusisha vyama vya soka vya mataifa, wachezaji wa mpira, walimu wa soka na wanaojitolea kuhudumu michezoni watasaidia kupata watu kupitia shughuli zinazohusisha mpira wa miguu.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud