Sheria ya uchaguzi ni hatua muhimu katika siku za usoni Somalia-UNSOM

3 Oktoba 2019

Mkutano wa wadau na Somalia umekamilika leo Jumatano katika mji mkuu Mogadishu huku washiriki akiwemo Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia James Swan akifuatilia hatua ambazo zimepigwa huku akizingatia pia changamoto zinazosalia na makubaliano ya vipaumbele katika siku zijazo.

Akizungumza katika mkutano huo Waziri Mkuu wa Somalia Hassan Ali Khayre amesema, “Somalia imepiga hatua kubwa. Tuko tayari kusonga mbele pamoja katika muda huu mfupi, pamoja na wawakilishi wa majimbo, bunge zote na viongozi wa kisiasa. Tunadhamiria kusonga mbele, kuhakisha kwamba hatua zilizopigwa hazitapotea.”

Ameongeza kwamba, “kwa mantiki hiyo katika kipindi kijacho, tutafanya kazi na vipaumbele fulani, ikiwemo kufanya uchaguzi wa wazi na huru na kuhakikisha amani wakati wa mpito, kukamilisha marekebisho ya katiba na kuimarisha usambazaji wa mamlaka, wakati huo huo kuzingatia hatua zilizopigwa na uwekezaji wa wadau wa kimataifa.”

Mkutano huo wa siku mbili umewaleta pamoja wawakilishi kutoka serikali kuu ya Somalia na wawakilishi wa serikali kutoka nchi zingine na mashirika mengine ya kimataifa.

Dhamira yao ya pamoja imeorodheshwa kupitia taarifa iliyotolewa mwishoni mwa mkutano huo wa siku mbili ambapo inasema, “wadau wa kimataifa wanatambua hatua ilizozipiga Somalia na inapongeza uongozi wa serikali kuu ya Somalia kwa hatua katika kutekeleza mabadiliko ikiwemo kuimarika kwa usimamizi wa fedha za umma na uzalishaji wa kipato, majadiliano kuhusu mpango mpya wa maendeleo kitaifa, mabadiliko katika usalama, operesheni zilizo zaa matunda kuhusu kuchukua maeneo yaliyokuwa yanashikiliwa na Al-Shabaab, ongezeko la uwasilishaji wa huduma za kijamii na hatua katika upatanisho mashinani.”

Taarifa hiyo imekwenda mbali zaidi na kusema, “wakati huo huo , kuna changamoto bado zinasalia, ikiwemo haja ya kuanzisha ajira na ukuaji wa kiuchumi, kuendelea kukabiliana na Al-Shaabab, kukbailiana na janga la kibinadamu na kujengea jamii mnepo, kuweka msingi kwa ajili ya siasa jumuishi na kuimarisha haki za binadamu, ushiriki na uwakilishi wa wanawake na walio wachache.”

Uwajibishwaji wa pamoja

Kuhusu makubaliano ya ufuatiliaji (MAF) kwa mwaka 2019 hadi 2020, serikali ya Somali na wadau wa kimataifa wamekubaliana kulenga juhudi kwa ajili ya maeneo ya kipaumbele kwa ajili ya hatua na raslimali kwa jili ya kufikia matokeo kabla ya Desemba mwakani.

Wadau wa kimataifa wamezingatia kwamba licha ya mafanikio yaliyopatikana, ushirikiano zaidi kati ya serikali kuu na serikali za majimbo ungeharakisha mchakato wa hatua zilizofikiwa.

Viongozi wa Somalia wamekubaliana kwamba ushirkiano kama huo ni muhimu kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa kisiasa, usalma na katika Nyanja za kiuchumi na hilo litahitaji dhamira binafsi ya viongozi wote mashinani na katika ngazi ya kitaifa.

Sheria ya mtu mmoja kura moja ni muhimu

Kuhusu sheria ya mtu mmoja, kura moja wakati wa uchaguzi mwishoni na mwaka 2021, taarifa imetaja namna ambavyo mamlaka ya serikali na usimamizi wa sheria wamedhamiria kupata sheria ya uchaguzi ifikapo Desemba mwaka huu.

Mapema katika majadiliano kuhusu siasa jumuishi, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini Somalia na mkuu wa Ujumbe wa Umoja huo nchini humo, James Swan amesisitiza umuhimu wa kuzingatia muda akisema, “upitishwaji wa sheria ya uchaguzi ni hatua ifautayo muhimu na tunafurahi kuona dhamira ya kuhakikisha kukamilika kwake kufikia mwisho wa mwaka huu, uwezekano wa kutofikia ahadi hiyo utahatarisha uchangishaji wa fedha muhimu na kuhatarisha muda wa uchaguzi.”

Aidha Bwana Swan ameongeza, “siasa jumuishi iwapo zitapatiwa uongozi unaohitajika na makubaliano yaliyofikiwa una uwezekano wa kuharakisha mchakato wa dhamira ya makubaliano ya ufuatiliaji.

Mabadiliko katika sekta ya usalama

Kuhusu mabadiliko katika usalama, taarifa imeainisha namna Somalia imedhamiria kujumuisha operesheni za sasa za kiusalama, kuanzisha operesheni zingine dhidi ya Al-Shabaab na kukamilisha mabadiliko katika eneo la usalama pamoja na haki na taasisi za haki za binadamu.

Mwaka 2020, mambo yote hayo kwa pamoja yatatambuliwa na kupangwa ili kuhakikisha kwamba washikadau wote wanaweza kupanga juhudi zao na raslimali kwa ajili ya maeneo waliokubaliana.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud